NA HAFSA GOLO
SERIKALI imewataka Maofisa wa Elimu wa Mikoa Zanzibar, kusimamia vipaumbele vilivyowekwa kwa ajili ya usimamizi wa mitihani ya majaribio (MOCO) katika kuhakikisha wanafunzi wa kidatu cha nne wanafanya mitihani hiyo kwa uadilifu na kuondokana na vikwazo vitakavyochangia kutofikia malengo ya mtihani huo.
Mkurugenzi Elimu Sekondari Asya Iddi, alieleza hayo alipokua akizungumza na gazeti hili ofisini kwake Mazizini Unguja, na kuwataka watendaji hao wasimamie majukumu yao kwa ufanisi huku wakizingatia sheria,kanuni na miongozo ya mitihani.
Alisema hatua hizo zitasaidia kufikia azma iliyokusudiwa katika kuwapima wanafunzi inavyostahiki na kufahamu jinsi walimu wa masomo walivyotekeleza majukumu yao ya kazi.
“Mitihani hii ya majaribio ni kielelezo tosha kinachosaidia kutoa vipimo vya kutambua namna ya athari na mapungufu yaliojitokeza kwa wanafuzi katika uwelewa wa masomo yao sambamba na hatua gani ya uwajibikaji kwa walimu hao”,alisema.