BEIRUT,LEBANON

BAADHI  ya maofisa wa mji wa Beirut wamewekwa katika kifungo cha nyumbani huku wakisubiri uchunguzi kuhusu mripuko mkubwa wa siku ya Jumanne uliopelekea zaidi ya watu 100 kuuawa.

Waziri wa Habari wa Lebanon Manal Abdul Samad Najd,alisema kuwa,kifungo cha nyumbani kitawashirikisha maofisa wote wa bandari, ambao walihusika katika suala la kuhifadhi amoniamu naitreti, wakiilinda na kusimamia usimamizi wake tangu Juni 2014.

Wakati huo huo,Wizara ya Afya ya Lebanon ilitangaza kuwa,idadi ya watu waliofariki dunia katika mripuko huo iliongezeka na kufikia wahanga 135 huku waliojeruhiwa wakiwa takriban elfu tano.

Mripuko huo ulitokea katika ghala nambari 12 la Bandari ya Beirut na kwamba sababu ya moto ni mada za miripuko ambazo zilikuwa zimehifadhiwa hapo.

Mripuko huo ulikuwa mkubwa kiasi cha kusikika kilomita nyingi kutoka eneo la tukio.

Taarifa zaidi kutoka mji mkuu wa Lebanon Beirut zinasema kuwa, mripuko huo ulisababisha hasara kubwa kwa nyumba za makaazi na pia katika idara binafsi na za serikali hasa majengo yaliyokuwa karibu na tukio hilo.

Kwa mujibu wa Rais Michel Aoun tani 2,750 za mada za amoniamu naitreti zinazotumika kwa utengenezaji wa mbolea na mabomu zilikuwa zimehifadhiwa katika bandari ya Beirut kwa muda wa miaka sita bila kuchukuliwa tahadhari za kiusalama.