NA MASANJA MABULA, PEMBA

UONGOZI wa Halmashauri ya Wilaya ya Micheweni umewataka wananchi kuyatumia maonyesho ya nane nane yanayoendelea katika viwanja vya Chamanangwe wilaya ya Wete, kwa ajili ya kujifunza taaluma zitakazowawezesha kulima  kwa kutumia kilimo chenye tija.

 Baadhi ya wananchi waliofika kwenye banda la maonyesho la Halmashauri ya Wilaya ya Micheweni walielezea kuvutiwa na taaluma ya kulima mboga mboga ambacho hakitumii udongo.

Othman Mbarouk Ali alisema taaluma ya kilimo bila ya kutumia udongo, kinaweza kumkomboa mwananchi wa kawaida kuongeza kipato chake.

“Hii ni taaluma mpya kwa hapa Pemba, hivyo naahidi kuitumia katika shamba langu lengo ni kuhakikisha uzalishaji unaongezeka”alifahamisha.

Naye Sharafa Juma Khamis, alisema kwamba, kilimo hicho kinatoa fursa kwa wananchi kujifunza kupitia maonyesho hayo, na kuahidi kuiendeleza kwa faida yake.

“Tumefika hapa na tumenufaika sana na elimu hii, naaimini nikitoka hapa nitahakikisha kilimo hichi nitakiendeleza na utanipunguzia suala la kununua mboga mboga kwa wafanyabiashara”alifahamisha.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Micheweni,, Hamad Mbwana Shehe, alisema kilimo cha mboga mboga bila ya kutumia udongo , mkulima kinaweza kumkombo mkulima kwa haraka tofauti ya njia nyengine za kilimo.

Alisema kilimo hichi kinakwenda kifuta malalamiko yanayotolewa na wakulima kwamba hawana maeneo ya kilimo.

“Faida ya kilimo hichi ni kwamba mkulima anatumia eneo dogo kwa kuzalisha na kipato chake ni kikubwa , hivyo sisi kama  Halmashauri tunaenda kuisambaza kwa wakulima vijijini”alisema.