JESHI la Marekani limedumu katika ardhi ya Ujerumani kwa miaka 75, ambapo wanajeshi hao walibakia nchini humo baada ya kumalizika kwa vita vya pili vya dunia.
Baada ya jeshi la Ujerumani kushindwa kwenye vita vya pili vya dunia wakati huo nchi hiyo ikiongozwa na dikteta Adolf Hitler, mkataba mmoja ulioilazimisha Ujerumani kuusaini ni Marekani kuweka ngome zake za kijeshi nchini humo.
Lengo la jeshi la Marekani kuwepo nchini Ujerumani katika miaka ya awali ni kukabiliana kwa haraka na madikteta wengine watakoafanana na Hitler, hata hivyo ulipofika wakati na baada ya vita baridi malengo yalibadilika.
Kwa mfano wakati wa vita baridi Marekani ililiweka jeshi lake liliopo nchini Ujerumani katika hali ya tahadhari kwani adui mkubwa wa wakati huo ilikuwa nchi ya shirikisho la soviet nchi ambayo kwa sasa inajulikana kama Urusi.
Baada ya kumalizika vita baridi, Marekani inalitumia jeshi lake lilipo Ujerumani kwa ajili ya vita katika maeneo mbalimbali inayopambana hasa katika eneo la mashariki ya kati.
Uwepo wa jeshi la Marekani nchini Ujerumani limezidisha ushirikiano wa dhati baina ya nchi hizo ambapo famialia za wanajeshi wa kimarekani na wananchi wa Ujeumani wanaishi kwa mashirikiano makubwa.
Wananchi wa Ujerumani nao wamekuwa wanufaika wakubwa kwa kupata ajira kwenye kambi za wanajeshi wa Marekani ambapo hadi mwaka 2019, inaelezwa kuwa kiasi cha raia wa Ujerumani 17,000 wameajirikia wakifanyakazi mbalimbali kwenye kambi za jeshi la Marekani.
Doa jeusi la ushirikiano baina ya Ujerumani na Marekani liliingia miaka 20 iliyopita wakati kansela wa Ujerumani wa wakati huo Gerhard Schröder na rais wa Marekani George W. Bush, walipohitilafiana dhida ya vita nchini Iraq.
Kansela Gerhard Schröder alikataa kata kata kuijumuisha nchi yake kwenye vita hivyo vilivyodaiwa sababu yake ni kuiadabisha Iraq kutokana na kumiliki silaha za maangamizi ya halaiki.
Katika miaka siku za hivi karibuni rais wa sasa wa Marekani, Donald Trump anatoa kauli za mara kwa mara zenye dhamira ya kutaka kuwaondosha wanajeshi wa nchi hiyo walioko Ujerumani.
Taarifa zinaeleza kuwa Marekani ina karibu wanajeshi wanaofikia 35,000 wengi wao wakiwa katika magharibi na kusini ya nchi hiyo, lakini kwa mujibu wa rais wa Marekani, nchi hiyo inapanga kuondosha wanajeshi wake wapatao 12,000.
Kuondolewa kwa wanajeshi hao kunaelezwa kwamba kutaipa nafasi Marekani kupanga mikakati yake kisheji barani Ulaya, ambapo ya wanajeshi 12,000 nusu wanajeshi 6,400 watarejeshwa nyumbani huku wengine wakipelekwa katika nchi washirika wa NATO kama vile Italia na Ubelgiji.
Trump alisema hatua ya kuwaondoa wanajeshi nchini humo inatokana na Ujerumani kushindwa kufikia malengo ya NATO hasa kutochangia bajeti ya ulinzi wa shirika hilo la kujihami.
Kwa kipindi kirefu, Trump analalamika kwamba washirika wa NATO wa Ulaya wanastahili kuongeza kiwango chao cha matumizi kwa ajili ya ulinzi wao wenyewe na kwamba Marekani haistahili kutegemea Marekani kubeba mzigo.
Huku Trump akipanga kuwaondosha wanajeshi wake, hata hivyo anakabiliwa na upinzani mkali nchini mwake ikiwemo bunge la nchi hiyo linaloeleza kuwa kuondolewa kwa wanajeshi hao kutaipa mwana Urusi kujiimaisha zaidi.
Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Mark Esper wakati anatangaza uamuzi huo, alisema kwamba hatua hiyo ni sehemu ya mpango wa muda mrefu wa kuhamisha wanajeshi wa Marekani katika eneo hilo.
Alisema “ni mkakati muhimu na uhamisho utakao kuwa na munafaa na ambao bila shaka yoyote utasaidia katika kufikia kanuni za msingi za kuimarisha Marekani”.

Hatua hiyo imepangiwa kugharimu serikali ya Marekani dola bilioni kadhaa na pia itapunguza uwepo wa wanajeshi wa Marekani nchini Ujerumani kwa zaidi ya asilimia 25.
“Ndege za kivita zitahamishwa hadi Italia huku baadhi ya wanajeshi huenda wakahamishwa Poland”, Esper alimesema.
Hata hivyo umauzi huo umekosolewa na maafisa wa Ujerumani, huku mwenyekiti wa kamati ya masuala ya mambo ya nje akisema kuwa hilo huenda likadhoofisha muungano wa NATO.
Na mkuu wa jimbo la Bavaria, Ujerumani, Markus Soeder, alisema anasikitishwa na uamuzi huo. “Hatua hiyo inakuwa mzigo kwa uhusiano kati ya Ujerumani na Marekani,” aliwaambia wanahabari.
Katibu mkuu wa jumuiya ya NATO, Jens Stoltenberg alisema kwamba Marekani ilijadiliana na nchi wanachama wa NATO kabla ya kutangaza hatua hiyo ya kuondoa wanajeshi wake nchini Ujerumani.
Hivi karibuni matokeo ya uchunguzi wa maoni uliofanywa nchini Ujerumani unaonyesha kuwa raia wa nchi huo wanaunga mkono kuondolewa kwa wanajeshi wa Marekani nchini mwao na pia wanataka Marekani iondoe silaha zake za atomiki katika ardhi ya nchi hiyo.
Uchunguzi huo wa maoni uliofanywa na taasisi ya YouGov umeonyesha kuwa asilimia 66 ya wananchi wa Ujerumani wanaunga mkono mpango wa kuondoa nchini humo silaha za nyuklia za Marekani na ni asilimia 19 tu wanaotaka silaha hizo za Marekani zisalie nchini humo.
Kwa mujibu wa matokeo ya uchunguzi huo wa maoni ya taasisi ya YouGov, karibu robo ya wananchi wa Ujerumani wanaamini kuwa vikosi vya usalama vya Marekani vinapasa kuondoka kikamilifu katika ardhi ya Ujerumani.
Marekani ina mpango wa kuzihamishia nchini Italia ndege zake za kivita aina ya F-16; ambazo sasa zipo katika jimbo la Rhineland-Palatinate huko Ujerumani.