WASHINGTON,MAREKANI
RAIS wa Marekani Donald Trump anataka kushinikiza Iran irejeshewe vikwazo kamili vya Umoja wa Mataifa.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Mike Pompeo,jana aliwasilisha mpango wenye utata unaolenga kuiwekea tena Iran vikwazo vya kimataifa, ambavyo viliondolewa kama sehemu ya makubaliano ya mkataba wa nyuklia wa mwaka 2015.
Hatua hiyo inaelezwa kwamba itazidisha mvutano wa kidiplomasia baina ya Marekani na washirika wake kwenye baraza la usalama la Umoja wa Mataifa.
China, Urusi, Uingereza, na Ufaransa ambazo zilitia saini mkataba wa nyuklia wa 2015 na wanachama wa kudumu wa baraza la usalama, zinapinga wazo la kuirejeshea Iran vikwazo.
Aidha Uingereza, Ufaransa na Ujerumani, zilisema Marekani haina tena usemi juu ya mkataba huo, baada ya kujiondoa miaka miwili iliyopita.