WASHINGTON,MAREKANI

SERIKALI ya Marekani imesema itaiendeleza asilimia 15 ya ushuru kwenye vifaa ya kampuni ya ndege vya Airbus pamoja na asilimia 25 kwenye bidhaa nyengine za Ulaya licha ya hatua zilizochukuliwa na Umoja wa Ulaya za kusuluhisha mzozo wa muda mrefu unaohusiana na ruzuku za kampuni hiyo.

Mwakilishi wa Marekani kwenye mazungumzo hayo Robert Lighthizer alisema Umoja wa Ulaya haujachukua hatua zozote za muhimu zainazoendana na maamuzi ya Shirika la kimataifa la biashara,WTO na Washington itaanzisha mchakato mpya wa kujaribu kufikia suluhu ya muda mrefu.

Ofisi ya Lighthizer ilisema itarekebisha orodha yake ya bidhaa za thamani ya dola bilioni 7.5 kutoka Ulaya zilizoathirika ili kuondoa baadhi ya bidhaa kutoka Ugiriki na Uingereza na kuongeza idadi sawa ya bidhaa kutoka Ujerumani na Ufaransa.