SERA za Marekani kwa sasa ni kuiwekea shindikizo kubwa Jamhuri ya kiislamu ya Iran, ambapo inataka kuhakikisha taifa hilo linarejeshewa vikwazo vyote vya kimataifa.

Marekani imeufahamisha rasmi Umoja wa Mataifa kuhusiana na matakwa yake ya vikwazo kwa Iran virudishwe, hali ambayo imesababisha upinzani kutoka kwa Urusi na wanachama wengine wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Kwa bahati mbaya sana hata nchi rafiki kwa muda mrefu na Marekani kutoka Ulaya nazo zimeonesha upinzani dhidi ya matakwa ya Marekani katika kurejesha vikwazo kwa Iran wakiitaja hatua hiyo kuwa kinyume cha sheria.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Mike Pompeo alimfahamisha rais wa Baraza hilo la Usalama akisema Iran imekiuka pakubwa mkataba wa mwaka 2015 wa nyuklia jambo linalotoa nafasi ya kuwekwa vikwazo hivyo kwa mara nyengine tena.

“Marekani haitokubali kamwe mfadhili mkubwa wa ugaidi duniani kununua na kuuza ndege, gari za kivita, makombora na silaha nyengine bila udhibiti. Vikwazo hivi vya Umoja wa Mataifa vitaendeleza marufuku ya kununua silaha,” alisema Pompeo.

Makataba unaoizuia Iran kununua silaha inamalizika Oktoba 18, ambapo pia chini ya mkataba huo Iran haiwezi kufanya majaribio ya makombora na urutubishaji wa madini ya urani.

Mara baada ya hatua hiyo ya Marekani naibu balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa, Dmitry Polyansky ameandika katika mtandao wa kijamii wa Twitter akiishambulia Marekani kwa kutoheshimu sheria na kufanya kile inachotaka bila kumshauri yeyote.

Tayari China na Urusi, wanachama wawili wa Baraza la Usalama wenye kura ya turufu wameshatangaza kupinga jitihada hiyo ya Marekani dhidi ya Iran.

Uingereza, Ufaransa na Ujerumani nchi ambazo ni wanachama wa mkataba wa nyuklia wa mwaka 2015, wameungana na Urusi kuipinga hatua hiyo ya Marekani licha ya kuwa nchi hizo za Ulaya ni marafiki wa Marekani, jambo linaloashiria kibarua cha Marekani katika suala hilo.

Marafiki hao wa Marekani walishangazwa na hatua za Marekani chini ya utawala wa Donlad Trump kuiondoa nchi hiyo kwenye mkataba wa nyuklia na Iran mnamo mwaka 2018.

Pamoja na kuishawishi sana Marekani, lakini Trump alisimamia maamuzi yake ya kuiondoa nchi yake kwenye mkataba huyo wa nyukilia na kuirejeshea tena vikwazo nchi hiyo iliyopo ghuba ya uajemi.

Akizungumzia hatua ya Marekani kushindikiza vikwazo vipya, balozi wa Iran kwenye umoja wa mataifa, Majid Ravanchi imeikosoa Marekani kwa hatua hiyo iliyochukua.

“Kulingana na hoja za kisheia, Marekani si mshiriki wa mkataba wa nyuklia na haina haki ya kukitumia kipengele cha kurudisha tena vikwazo na tafsiri yake ya azimio 2,231 haiwezi uubadilisha ukweli”, alisema Majid.

Rais wa Iran, Hassan Rouhani ameonya kuwa nchi yake itajibu iwapo Baraza la Usalama litarefusha vikwazo hivyo vya silaha lakini hakuainisha hatua watakazochukua.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Usimamizi wa Niashati ya Nyuklia limeripoti kuhusiana na Iran kwenda kinyume na makubaliano hayo ingawa Iran yenyewe inasema hiyo inatokana na Marekani kukiuka makubaliano hayo kwa kujiondoa na kisha kuiwekea Iran vikwazo vikali vya kimataifa.

Hata hivyo wachambuzi wanaeleza kuwa Marekani inatarajiwa kushindwa na huenda ikauweka rehani mkataba wa nyuklia kati ya Iran na mataifa sita yenye nguvu ambao tayari utekelezaji wake unasuasua.

Pendekezo jipya lililowasilishwa na Marekani linataka vikwazo hivyo kurefushwa bila ya kikomo ikisema iwapo vitaondolewa, Iran itakuwa msambazaji wa silaha bila kuzingatia maadili ya kimataifa.

Taarifa zinaeleza kuwa iwapo pendekezo hilo litashindwa, Marekani imetishia kutengua kipengele cha mkataba wa nyuklia kinachoruhusu washirika wa mkataba huo kuutuhumu upande mwingine kwa kutotekeleza masharti ya mkataba.

Kwa sasa kuna wasiwasi mkubwa kwamba juhudi hizo mpya za Marekani huenda zitauvuruga mkataba wa Vienna uliolenga kuizuia Iran kutengeneza silaha za nyuklia kwa ahadi ya kuondolewa vikwazo vikali vya kiuchumi.

Hata hivyo, wafuatiliaji wa suala hilo wamesema Marekani haina haki ya kutumia kipengele hicho kwa sababu rais Donald Trump aliiondoa nchi yake kutoka mkataba wa nyuklia na Iran mwaka 2018 na kurejesha vikwazo vya Marekani dhidi ya taifa hilo la kiislamu.

Makubaliano ya nyuklia yaliyofikiwa kati ya Iran, Uingereza, China, Ufaransa, Ujerumani, Urusi na Marekani utekelezwaji wake ulianza kuyumbayumba baada ya Marekani kujitoa na Tehran kuanza kukiuka vipengele vya mkataba.