NA MARYAM SALUM, PEMBA
KUTOWASILI kwa mashahidi wa kesi inayomkabili aliyekuwa ‘bosi’ wa
Shirika la Biashara la Taifa Zanzibar ‘ZSTC’ Wilaya ya Mkoani, Seif
Suleiman Kassim, anayekabiliwa na tuhuma za kubaka mwanafunzi,
kumelazimika kuahirisha kwa mara nyingine tena baada ya upande wa
mashtaka kutopokea mashahidi wa shauri hilo.
Akiwa mahakama ya mkoa Chake Chake, Mwendesha mashtaka kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka, Mohamed Ali Juma alidai shauri hilo lipo kwa
ajili ya kusikilizwa, ingawa upande wao hawajapokea mashahidi.
Alidai kuwa kutokana na kutowapokea mashahidi hao, ni vyema mahakama
hiyo kuliahirisha shauri hilo na kulipangia tarehe nyingine kwa ajili
ya kusikilizwa.
“Mheshimiwa hakimu shauri hili lipo kwa ajili ya kusikilizwa, lakini
kwa upande wetu, hatujakupokea mashahidi, hivyo ni vyema likahirishwa
na kupangiwa tarehe nyengine ingawa mtuhumiwa husika yupo mahakamani
anasubiri mwendelezo wa shauri lake”, alidai.
Hakimu wa shauri hilo, Adull-razak Abdull-kadir Ali, hakuwa na pingamizi
juu ya ombi hilo, na kisha kuliahirisha na kutaka lirudi tena
mahakamani hapo Septemba 15, mwaka huu, kwa ajili ya kusikilizwa.
Mwendesha Mashitaka alidai, shauri la Mtuhumiwa huyo linawakilishwa na
Wakili Abeid Mussa Omar, pamoja na wakili Ali Hamad Mbarouk, ambapo pia
nao waliridhia juu ya kuahirishwa kwa shauri hilo.
Awali ilidaiwa kuwa, mshtakiwa huyo Seif Suleiman Kassim miaka 58 wa
Jiondeni Mkoani, alimtorosha mtoto wa miaka 13 ambae ni mwanafunzi,
katika tarehe isiofahamika mwezi wa Aprili mwaka jana, majira ya saa
6: 00 mchana, eneo la Bandarini Mkoani Pemba.
Ilidaiwa kuwa bila ya halali, alimtorosha mtoto huyo wakati alipokua
anakwenda skuli na kisha kumuingiza kwenye ofisi aliyokuwa akifanyia
kazi ya ‘ZSTC’ iliyopo Bandarini Mkoani.
Hilo ni kosa kinyume kifungu cha 113 (1) (a) cha sheria ya Adhabu
namba 6 ya mwaka 2018, sheria ya Zanzibar.
Kosa la pili linalomkabili, ni la ubakaji wa mtoto huyo huyo, ambapo
kufanya hivyo ni kinyume na kifungu cha 108 (1), (2) (e) na kifungu
cha 109 (1) cha sheria ya Adhabu no 6 ya mwaka 2018, sheria ya
Zanzibar.