NA ASIA MWALIM
VIONGOZI wa shehia nchini wametakiwa kuwa mstari wa mbele kuhakikisha wanatatua matatizo yaliyomo ndani ya shehia zao, ili kufanikisha maendeleo ya shehia.
Wito huo umetolewa na Sheha wa shehia ya kwalinatu Salum Shaban Mzee, alipokua akizungumza na gazeti hili huko shehia ya kwaalinatu Wilaya ya Mjini Unguja.
Alisema kumekuwa na baadhi ya viongozi wa shehia hususan masheha wapo nyuma katika kushiriki kuondoa changamoto zilizokuwemo ndani ya shehia zao, ikiwemo uuzaji na utumiaji wa dawa za kulevya.
Alifahamisha kuwa jamii imekumbwa na dimbwi kubwa la vijana ambao wamejiingiza katika utumiaji wa dawa za kulevya, ambao wameacha kujituma, kujitafutia kipato halali, hivyo hupelekea kuwa tegemezi jambo ambalo linarudisha nyuma maendeleo yao na shehia kwa ujumla.
Sheha huyo amesema ikiwa viongozi hao wataweza kulipa kipaumbele suala la kutatua changamoto za shehia basi vikundi viovu ambavyo vipo ndani ya shehia vingeweza kupungua, na kuwanyima vijana hao fursa za kufanya matendo mabaya ikiwemo utapeli, wizi wa mazao na mifugo.
Aidha amesema wameweza kupunguza uingizaji wa dawa za kulevya katika shehia yao kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi pamoja na askari jamii katika kuondoa tatizo hilo.