TRIPOLI, LIBYA

WAZIRI  wa Mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas amesema mataifa ya kigeni yanayoendelea kukiuka marufuku ya silaha inayolenga kukomesha uingizaji wa silaha nchini Libya yatakabiliwa na vikwazo vipya.

Maas alitoa kauli hiyo wakati wa ziara yake katika nchi ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), ambayo inafuatia ziara yake aliyoifanya mwanzoni mwa wiki hii nchini Libya na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu Fayez Serraj ya namna ya kukomesha vita vya kugombania madaraka baina ya serikali yake na Khalifa Haftar.

Serraj anaungwa mkono na Uturuki na Qatar wakati Haftar akiungwa mkono na Misri, Urusi na UAE.

Umoja wa Ulaya ulizindua operesheni ya baharini inayojulikana kama IRINI katika juhudi za kuzuia usambazaji wa silaha katika taifa hilo lililokumbwa na machafuko.