NA KHAMISUU ABDALLAH

KATIBU wa Kamati Maalum, Idara ya Itikadi na Uenezi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Catherine Peter Nao, amesema mwishoni mwa wiki hii chama chake kitakamilisha mchakato wa uteuzi wa wagombea wa nafasi mbalimbali katika vyombo vya dola.

Alisema kuwa kipindi hicho kkinaweza kuwa kigumu na kuwasononesha wagombea waliokwenda kinyume na taratibu zilizowekwa na chama hicho.

Alisema hiyo ni kutokana na vikao vya sekretarieti ya Kamati Kuu ya CCM kilichoanza jana na kukamilika leo jijini Dodoma, kuanza kujadili wagombea wote walioomba nafasi za ubunge, uwakilishi na udiwani ili kutoa mapendekezo katika vikao vya juu.

Akizungumza na Zanzibar Leo kwa njia ya simu akiwa jijini Dodoma, Catherine alisema, Agosti 18 mwaka huu, Kamati ya Usalama na Maadili ya CCM Taifa itakaa na kufuatiwa na kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu itakayokutana Agosti 19 mwaka huu.

Aliongeza kuwa mchakato wa uteuzi utahitimishwa Agosti 20 mwaka huu wakati Halamshauri Kuu ya Taifa itakapokutana kufanya uteuzi wa mwisho kwa wagombea wa nafasi za ubunge, uwakilishi na udiwani.

“Baada ya siku hiyo (Agosti 20) kila mgombea atajua kama yumo au hayumo maana chama kilisema mapema kwamba kila mgombea hakuna kucheza faulu, hakuna rushwa na wala kufanya kampeni mapema,” alisema Catherine. 

Sambamba na hayo, aliwataka wanachama na wananchi kufahamu kuwa ndani ya CCM mtu hapitishwi kwa kura bali anarudishwa kwa vikao baada ya kuzingatia mambo mengi ikiwemo uadilifu wa mgombea.

“Mtu asitegemee amepata kura nyingi akaona kama atarudishwa, hapana vikao vya chama ndivyo vitakavyomrudisha, watu waliozingatia maadili ya chama na wakayafuata basi wategeee mazuri na wale ambao walifanya faulu na kufanya mambo ambayo yalikatazwa basi watachuma walichokipanda,” alibainisha Katibu Catherine.

Alisema wiki hii ni wiki ya kucheka na kusononeka kwa wagombea wote waliokwenda kinyume na taratibu zilizowekwa na chama hicho katika kuwapata wagombea watakaogombea katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28.