Hatma yao kuamuliwa Dodoma

Vikao vya matayarisho vyamaliza kazi 

NA KHAMISUU ABDALLAH

HATIMAYE Chama cha Mapinduzi (CCM) kinatarajia kupitisha majina ya wagombea wa nafasi ya uwakilishi Agosti 30 mwaka huu jijini Dodoma.

Katibu wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar, Catherine Peter Nao, alisema uamuzi huo umefikiwa baada ya mgombea urais wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli kurejesha fomu na chama hicho kuzindua kampeni Agosti 29 jijini humo.

Alisema awali mchakato wa kuwapitisha wagombea hao kwa kamati kuu ulikuwa ufanyike ofisi kuu ya CCM Kisiwandui Zanzibar, lakini kutokana na ratiba hiyo wagombea hao watapitishwa na kikao hicho kwa niaba ya halmashauri kuu ya Taifa jijini humo.

“Tumeona kwa sababu tunazindua kampeni siku hiyo haina haja ya kuja huku, tutamaliza huko huko kwa wagombea wetu wa nafasi ya uwakilishi,” alisema.

Catharine, alisema, tayari vikao mbalimbali vimeshaanza kukaa ikiwemo sekretarieti ya kamati Maalum iliyokaa Agosti 24 na kuchambua majina ya wagombea hao na Agosti 26 itakaa kamati ya maadili na Agosti 27 itakaa kamati maalum kwa ajili ya kupendekeza majina ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi. 

“Vikao vyengine vitakuwepo isipokuwa halmashauri kuu ya Taifa na mchakato wa wagombea utafanywa na kamati kuu kwa niaba ya halmashauri kuu ya Taifa na kila mgombea atajua ni mwakilishi wa jimbo gani siku hiyo,” alisema.

Akizungumzia wagombea wa nafasi ya ubunge alisema tayari wagombea wote walioteuliwa wametimiza taratibu za uchukuaji na urejeshaji wa fomu katika tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC). 

Hivyo, aliwaomba wanaCCM na wananchi kuwa watulivu na chama kitawateuwa wagombea watakaopeperusha bendera katika uchaguzi mkuu wa oktoba 28 mwaka huu kwa tiketi ya CCM.

Hapo jana kamati maalum ya halmashauri kuu ya CCM Zanzibar chini ya uwenyekiti wa Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi walikutana mjini Zanzibar.

Pamoja na mambo mengine kikao kilipokea na kujadili taarifa ya mapendekezo ya wanaCCM walioomba kuteuliwa nafasi ya ujumbe wa Baraza la Wawakilishi, kutoka katika majimbo na nafasi ya uwakilishi viti maalum mikoa ya Zanzibar.

Kikao hicho ni maalum kwa mujibu wa matakwa ya Katiba ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 1977 toleo la 2017, ibara ya 108 na 109 (1), (7).

Aidha Chama cha Mapinduzi kimeeleza kuwa kikao hicho ni miongoni mwa vikao vyake vya uongozi vya kitaifa vinavyofanyika kwa mujibu wa kanuni na miongozo ya chama hicho.