NAIROBI, Kenya

NYANJA ya Raga ya Kenya inaomboleza kifo cha mchezaji Ian Waraba ambaye aliaga dunia siku ya Jumamosi, baada ya kuzama kwenye bwawa la Wamuini mjini Kitale, Kaunti ya Trans Nzoia.

Kwa mujibu wa ripoti ya kituo cha Polisi cha Kiminini, mchezaji huyo mwenye miaka 22, wa Kenya Harlequins alikuwa ameandamana na marafiki zake kwenye bwawa hilo kuogelea wakati kisa hicho kilitokea.

Wapiga mbizi kutoka Shirika la Msalaba Mwekundu tawi la Kitale, waliopoa mwili wa Waraba kutoka kwenye bwawa hilo siku ya Jumapili, Agosti 9.

Kenya Harlequins ilimuomboleza mchezaji huyo chipukizi kama aliyekuwa na bidii na alikuwa anakaribia kushirikishwa kwenye timu ya kwanza.

Waraba alijiunga na Harlequins mwaka jana na kucheza kama mchezaji wa kutegemewa katika timu ya tatu kabla ya kufuzu kuingia timu ya pili ambapo alishiriki kwenye mtanange wa Eric Shirley Shield.

 Bado mpango wa mazishi waendelea huku familia yake ikiomba msaada wa kumuandalia mazishi ya hadhi yake.