NA HUSNA MOHAMMED

AKIWA mmoja wa watu waliokaribu sana na Mwanamuziki nyota wa kizazi kipya Tanzania, Afrika Mashariki na dunia kwa ujumla, Ali Saleh (Ali Kiba) ameweza kumtambulisha vyema hapa Zanzibar kwa shughuli mbalimbali anazozifanya.

Huyo si mwengine bali ni Rashid Khalfan Ali, ambae ni kampeni Meneja wa Ali Kiba ambae hujumuika nae kwenye matamasha mbalimbali, kwenye kutoa misaada ya shughuli za kijamii na baadhi ya shughuli za Serikali na Chama hapa Zanzibar n ahata Tanzania kwa ujumla.

“Niko karibu nae sana Ali Kiba akija hapa Zanzibar mimi ndie kampeni meneja wake kwenye maonesho, matamasha, sherehe za chama na Serikali na hata wakati akirekodi kazi zake”, alisema Rashid.

Akizungumzia kuhusu ushiriki wake kwa shughuli za hivi karibuni, Rashid alitaja kuwa ni pamoja na mapokezi ya Dk. Hussein Ali Mwinyi, mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Mapinduzi.

“Kwanza tulikuwa nae pamoja Dodoma wakati wa uteuzi wa mgombea rais Zanzibar kupitia CCM, baadae alishiriki katika utambulisho wa mgombea huyo makao makuu ya Chama Kiswandui mjini Unguja”, alisema.

Aidha shughuli nyengine ambazo ameziratibu Rashid ni ya upigaji wa Fashfashi kwenye viwanja vya Maisara ambazo zilikuwa za mkesha wa Sherehe za Mapinduzi zilizofanyika Januari 11 mwaka huu.

Mbali na uratibu wa shughuli za msanii Ali Kiba, Rashid pia ni mwanaharakati wa jumuiya mbalimbali zisizo za kiserikali na za kiserikali kama ZASOSE, jumuiya ya kuratibu safari za kitaifa na kimataifa katika mamlaka ya anga Zanzibar nakadhalika.

“Pia nikiwa na Ali Kiba chini ya program ya Unforgotable tour, amekuwa akizisaidia nyanja ya elimu, michezo afya pamoja na utalii.

Akizungumzia kuhusu sekta ya afya, Timu meneja huyo, alisema ana mpango kwa Ali Kiba hapa Zanzibar akiongozwa naye timu meneja wake hapa visiwani Rashid Khalfan kusaidia huduma mbalimbali za kijamii ili kuona wanajamii wanafaidika na fursa za msanii huyo.

Alisema kuwa kabla ya hapo yeye akiwa na Ali Kiba, walikutana na makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi na kuzungumza nae juu ya mpango wake wa kusaidia huduma za kijamii.

“Mipango yote ilifeli mara tu baada ya kuibuka kwa ugonjwa wa corona hapa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla lakini kwa sasa tunatafuta njia ya kufanya baada ya kupungua corona”, alisema.

AFYA

Pamoja na mambo mengine, alisema kuwa kwanza wanatarajia kuweka kambi ya uchunguzi na matibabu ya afya kwa maradhi ya malaria, kisukari, shinikizo la damu na uchunguzi wa maradhi ya ebola kwa kuwashirikisha madaktari bingwa wa maradhi hayo.

“Kwa upande wa kambi ya madawa watu watapewa dawa mbalimbali kulingana na uchunguzi utakaofanywa na kambi ya matibabu sambamba na kupewa ushauri wa kiafya na hasa juu ya ugonjwa wa ebola”, alisema timu meneja huyo.

ELIMU

Aidha alisema msanii Kiba pia anasaidia nyanja ya elimu kwa vijana ambao wamemaliza elimu ya juu ambao hadi sasa hawajaweza kujiajiri kwa vijana.

“Ali Kiba ana mpango wa kuwajengea ndoto wanafunzi vijana wa vyuo vikuu na kuwashukuru watu mbalimbali waliomuunga mkono katika mambo ya muziki wakati akiwa anatembelea mikoa mbalimbali na baadhi ya sehemu tayari ameaanza”, alisema.

“Kabla ya corona alifanya ziara katika kijiji cha Dunga na kuonana na wanafunzi wa kidato cha nne na kuwapa motisha ya kuchakarika kimaisha na kuwa na malengo mbalimbali ya kimaisha”, aliongeza.

Sambamba na hilo lakini msanii huyo ataimarisha mchezo wa mpira wa miguu kwa makubaliano ya wahusika wa timu ili kuona vijana wanajiimarisha katika michezo mbalimbali.

MICHEZO

“Atatengeneza timu za kirafiki katika mikoa atakayotembelea na pia atatoa burdani kwa wananchi ambapo hata Zanzibar watafaidika na unforgettable tour ya msanii huyo”.

Aidha alisema kupitia mchezo wa mpira wa miguu wa hisani kati yake na mchezaji nyota wa Tanzania wa mpira wa miguu Mbwana Ali Samatta, alichezesha mechi hivi karibuni ambapo fedha zilizopatikana ziliwasaidia watoto wenye mahitaji maalumu hasa wenye matatizo ya moyo.

UTALII

Kuhusiana na utalii, Rashid alimtaja Kiba kuwa ni balozi wa kuitangaza Zanzibar kiutalii kwa kiasi kikubwa ataweza kuisaidia Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia usanii wake ili kujulikana Zanzibar katika uso wa dunia.

“Nahii itasaidia pale ambapo amefanya albamu yake moja kwenye jengo la ‘Beit el Ajaib lililoko Forodhani Mji Mkongwe mjini Unguja, albamu ile itaitangaza vizuri Zanzibar”, alijisifu Rashid.

Aidha alisema Kiba alitunukiwa cheti cha ubalozi wa utalii wa ndani na waziri wa Habari, Utalii na mambo ya kale, Mahmoud Thabit Kombo, hivyo anaamini kuwa ataifanyia kazi nyanja hiyo kwa kuwa ameonesha nia ya dhati kushirikiana na serikali kwa hilo”, alisema Rashid.

“Tulikuwa na mipango lukuki na Kiba kwa misaada mbalimbali kwa Zanzibar lakini Ugonjwa wa Corona uliotokea ulisababisha baadhi ya mambo kukwazika, lakini madam nia tunayo tutafanya wakati wowote kuanzia sasa”, alisema.

 “Ameanza kutembelea mikoa mbalimbali ya bara na Zanzibar ili kuona mahitaji halisi na kuweza kuutumia usanii wake kwa lengo la kuwasaidia vijana awamu kwa awamu.

Alisema lengo la mpango wa Unforgetable tour ni kulipa fadhila kwa watanzania ikiwemo mashabiki wa muziki wa kizazi kipya, hivyo katika kufanikisha mradi huo alizitaka taasisi mbalimbali kumuunga mkono ili kuisaidia jamii ya kitanzania.   

Huyo ndie Rashid Khalfan ambae ni Meneja wa Ali Kiba hapa Zanzibar, ambae amezaliwa mwaka 1956 hapa Zanzibar na kuanza elimu yake ya msingi na ile ya sekondari kuipatia Tanzania bara.

Baadae Rashid alipata elimu ya juu ya masuala ya fedha huko Brimigham nchini Uingereza.

Aidha alikuwa mtumishi wa Serikali katika wizara ya fedha na Mipango Zanzibar kwa takriban miaka 40 hadi alipostaafu kwake miaka michache iliyopita.