MADRID,UHISPANI
MFALME wa zamani wa Uhispania Juan Carlos, ameamua kuihama nchi hiyo,kwa lengo la kuunusuru ufalme baada ya mkururo wa tuhuma za ufisadi dhidi yake.
Mfalme huyo aliyewahi kuwa mashuhuri sana nchini mwake, anaripotiwa kwamba tayari ameshaondoka Uhispania, ingawa vyombo vya habari vya huko havijasema alipokwendea.
Tamko la kasri ya kifalme lililotolewa limeinukuu barua ya Juan Carlos kwa mwanawe na mfalme wa sasa, Filipe, akisema kwamba anataka kumuwezesha mwanawe huyo kuongoza kwa salama licha ya hasira za umma juu ya masuala ya maisha yake binafsi.
Kwa wiki kadhaa sasa, shinikizo limekuwa likiongezeka kwa wote wawili, baada ya waendesha mashitaka wa nchi hiyo na wa Uswisi kuanza kuchunguza tuhuma za rushwa dhidi yao.
Uamuzi huo unatarajiwa kuwagawa Wahispania kati ya wale wanaotaka abakie nchini kukabiliana na mashitaka na wale wanaodhani mfalme huyo wa zamani, mwenye miaka 82 alikuwa sahihi kuondoka.