NA SAIDA ISSA, DODOMA
MFUMKO wa bei wa taifa kwa mwaka ulioishia mwezi Julai mwaka huu umeongezeka kidogo hadi asilimia 3.3 kutoka asilimia 3.2 kwa mwaka ulioishia mwezi Juni mwaka huu.
Hali hiyo inamaanisha kuwa kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia mwezi Julai mwaka huu imeongezeka kidogo ikilinganishwa na kasi iliyokuwepo kwa mwaka ulioishia mwezi Juni mwaka huu.
Hayo yalibainishwa na Kaimu Mkurugenzi wa sensa na Takwimu za Jamii, Ruth Minja alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma.
Alisema kuwa kuongezeka kwa mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia mwezi Julai mwaka huu kumechangiwa na kuongezeka kwa bei za baadhi za vyakula na baadhi zisizo za vyakula kwa kipindi kilichoishia mwezi Julai mwaka huu zikilinganishwa na bei za mwezi Julai mwaka jana.
“Baadhi ya bidhaa za vyakula zilizoongezeka bei kwa mwezi julai mwaka huu zikilinganishwa na bei za mwezi Julai mwaka jana ni pamoja na unga wa mahindi kwa asilimia 7.9, mtama kwa asilimia 4.8, unga wa muhogo kwa asilimia 3.0, dagaa kwa asilimia 3.8, matunda kwa asilimia 4.0 na mbogamboga kwa asilimia 9.6”, alisema.
Kwa upande mwingine baadhi ya bidhaa zisizo za vyakula ziliongezeka bei kwa mwezi Julai mwaka huu zikilinganishwa na bei za mwezi Julai mwaka jana ni pamoja na mavazi kwa asilimia 2.8, gesi ya kupikia kwa asilimia 5.9, samani kwa asilimia 2.7, gharama za utengenezaji na ukarabati wa nyumba kwa asilimia 6.2 na mkaa kwa asilimia11.6.
Alisema kuwa mfumko wa bei bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwezi Julai mwaka huu umebaki kuwa asilimia 3.8 kama ilivyokuwa kwa mwaka ulioishia mwezi Juni mwaka huu.
Aidha alisema kuwa hali ya mfumko wa bei kwa nchi za Afrika Mashariki kwa mwaka ulioishia mwezi Julai mwaka huu ni Nchini Kenya mfumko wa bei kwa mwaka ulioishia mwezi Julai mwaka huu umepungua hadi asilimia 4.36 kutoka asilimia 4.59 kwa mwaka ulioishia mwezi Juni mwaka huu.