NAIROBI,KENYA
NJAA kubwa na utapiamlo vinawakaribia mamilioni ya wakimbizi katika eneo la Afrika Mashariki baada ya mgao wa chakula wanaoutegemea kutoka shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula Duniani (WFP) kupunguzwa zaidi.
Taarifa ya WFP ilieleza kuwa, changamoto za janga la corona au COVID-19 zilisababisha ufadhili muhimu kutoka kwa wahisani kupunguzwa.
Tayari shirika hilo lilikuwa limeshalazimika kupunguza mgao wa chakula au fedha hadi asilimia 30 kwa wakimbizi zaidi ya milioni 2.7 nchini Ethiopia,Uganda, Kenya, Sudan Kusini na Djibouti.
Aidha mpango wa chakula Duniani (WFP), utalazimika kupunguza zaidi mgao unaotoka katika miezi ijayo endapo haitapokea kwa wakati fedha zaidi kutoka nchi wahisani.
Akizungumzia changamoto hiyo Mkurugenzi wa WFP wa kanda ya Afrika Mashariki Michael Dunford alisema wakimbizi wako katika hatari kubwa ya kusambaa kwa janga la COVID-19 kwa sababu wanaishi katika mrundikano mkubwa makambini ambako pia hakuna huduma za kutosha za malazi, afya na fursa ya maji safi na salama.
Ofisa huyo wa WFP aliongeza kuwa wakimbizi wanakabiliwa na changamoto nyingi kubwa zaidi ikiwa ni virusi vya corona na athari za kiuchumi na kijamii zilizosababishwa na janga hilo, huku wanawake, watoto na wazee wakitaabika zaidi na kuwa katika hatari ya kupata utapiamlo kutokana na lishe duni.
Hivi sasa WFP inahitaji dola milioni 323 ili kusaidia mamilioni ya wakimbizi ukanda huo wa Afrika Mashariki kwa miezi sita ijayo, ombi likiwa ni asilimia 22 zaidi ya ilivyokuwa wakati kama huu mwaka jana.