NA ASIA MWALIM
MTU mmoja amefariki dunia baada ya kukutwa chumbani kwake akiwa amejinyonga kwa kutumia shuka la kitanda.
Kamanda wa Polisi Mkoa Mjini Magharibi Unguja (ACP) Awadh Juma Haji, aliyasema hayo alipokua akizungumza na waandishi wa habari huko Ofisini kwake Mwembemadema Mjini Zanzibar.
Kamanda Awadhi alimtaja marehemu huyo alijulikana kwa jina la Muhammed Abdalla Said (24) mkaazi wa Fuoni Kimara, Wilaya ya Magharibi ‘B’ Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.
Alifahamisha kuwa Marehemu alifanya tukio hilo Agosti 14 mwaka huu majira ya saa 11:00 jioni huko maeneo ya Fuoni, ambapo alikua peke yake ndani ya nyumba, wakaazi wengine wanaoishi humo waliondoka siku hiyo na baada ya kurudi walimkuta marehemu ananinginia kwenye boriti na tayari amefariki.
Alisema kuwa baada ya tukio mwili wa marehemu ulifikishwa hospitali ya Mnazi mmoja kwa uchunguzi wa kidaktari na baadae kukabidhiwa jamaa zake kwa ajili ya mazishi.