Uwanja wa Amaan wafanyiwa matengenezo makubwa
Mao Zedong wajengwa upya, viwanja vya mawilaya vyang’arishwa

ZASPOTI

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya Uongozi wa Awamu ya Saba ya Dk.Ali Mohamed Shein, imeendelea kuimarisha miundombinu mbali mbali ikiwemo viwanja vya michezo.
Ikiwa tayari Zanzibar ina viwanja vitatu vikubwa vya michezo ukiwemo uwanja wa Amaan, Gombani na Mao Zedong.


Tayari uwanja wa Gombani Pemba umefanyiwa matengenezo makubwa kwenye eneo la kuchezea na sehemu ya majukwaa huku Mao Zedong ukijengwa upya na kurudishiwa haiba yake kama ambavyo ulivyong’ara miaka ya 1950.


Lakini pia serikali ya Dk.Shein, inaendelea kuiimarisha uwanja wa Amaan kwa kuweka nyasi bandia mpya sehemu ya kuchezea baada ya matengenezo ya kuyang’arisha majukwaa, lengo ikiwa ni kurejesha hadhi ya uwanja huo ambao ni miongoni mwa viwanja bora nchini Tanzania.


Katibu Mkuu wa Wizara Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Omar Hassan ‘King’, anasema, matengenezo hayo yameshafikia asilimia 75 huku kazi ikiendelea kwa kasi na ufanisi zaidi.
Anasema, mfumo unaotumika kwa sasa ni zege maalum ili uwanja huo uweze kufanyakazi vizuri.


“Napenda kumpongeza Rais wa Zanzibar, Dk.Ali Mohamed shein, kwa kujitolea kuinua sekta ya michezo, sekta zote anafanya vizuri, lakini, hii ya michezo ina nafasi ya kipekee”, alisema, King.
“Ni imani yetu kwamba sasa tutaimarisha michezo ikiwa pamoja na kuchagua viongozi wa michezo watakaohakikisha wanainua sekta hiyo yenye kupendwa na wengi”.
“Tunahitaji viongozi watakaokuwa na uwezo wa kuinua michezo ili kuendana kasi ya kidunia kwenye sekta hiyo”.


“Lengo ikiwa ni kutumia vyema huu uwekezaji uliowekwa na serikali kuanzia viwanja vya michezo na maeneo mengine ya kimichezo”.
Hivi karibuni akizungumza na uongozi wa Wizara Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo wakati ilipowasilisha taarifa ya utekelezaji wa mpango kazi wa mwaka 2019/2020 na mpango kazi wa 2020/2021, Dk. Shein, alisema, Zanzibar inahitaji kuwa na uwanja mkubwa wa kisasa utakaowezesha kufanyika shughuli mbali mbali za kitaifa.


Alisema uwanja wa aina hiyo, utakaokuwa na uwezo wa kufanyika matukio mbali mbali ya kitaifa, kama vile gwaride pamoja na michezo ya aina tofauti, ikiwemo mpira wa miguu, utasaidia katika jitihada za kuinua sekta ya michezo nchini.


Alisema uwanja wa Amaan hauwezi kukidhi mahitaji ya wakati huu na hivyo ipo haja ya kuangaliwa maeneo ya nje ya mji, likiwemo eneo la Tunguu ambalo limekusanya taasisi mbali mbali na wizara za serikali na kuwa katika mpango huo.


Waziri wa Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Balozi Ali Abeid Karume, alielezea baadhi ya mafanikio yaliopatikana na wizara hiyo katika kipindi hicho ambapo uimarishaji wa uwanja wa Amaan kupitia bajeti ya 2019/2020.


Alisema kazi za ujenzi wa viwanja katika wilaya za Unguja ikiwemo cha Mkokotoni (wilaya Kaskazini “A”), kinachojengwa na Wizara Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji kupitia Wakala wa Barabara Zanzibar zimeanza.
Alisema wizara tayari imepokea makisio ya ujenzi wa kiwanja kiliopo Kama (wilaya Magharibi ‘A’), huku hatua za kuomba fedha Wizara ya Fedha na Mipango ikiwa tayari zimechukuliwa.


Waziri Karume alibainisha wizara hiyo imeanza kukisaidia kituo cha michezo cha JKU (JKU Sports Academy) kwa kukipatia vifaa mbali mbali vya michezo, vitanda, magodoro pamoja na kugharamia huduma mbali mbali za vijana waliopo kituoni hapo, ambapo vijana 130 wananufaika na programu hiyo wakiwemo wachezaji wa mpira miguu na waamuzi wadogo.

HISTORIA YA UWANJA WA AMAAN

Uwanja wa Amaan mjini Unguja ni wa kihistoria, japo wengi hawafahamu. Ulijengwa kwa msaada wa Serikali ya China na ulifunguliwa mwaka 1970, ukiwa ni mradi mkubwa wa nchi wa viwanja vya michezo barani Afrika.
Michezo na sherehe nyingi hufanyika uwanjani hapo. Sherehe kubwa ya kihistoria ilifanyika Februari 5, 1977 wakati vyama vya TANU na Afro Shirazi vilipoungana na kuzaliwa Chama cha Mapinduzi (CCM).


Uwanja huo ulifungwa kwa muda na kufanyiwa ukarabati mkubwa kabla ya kufunguliwa tena mwaka 2010 na una uwezo wa kukaa watu 15,000.
Pia ni uwanja wa kwanza kuchezewa mechi usiku hapa nchini Tanzania.
Kuanzia Septemba 17, 1967, Rais wa Kwanza wa ASP, Hayati Abeid Amani Karume, alianza mbio za ujenzi wa uwanja wa Amaan, baada ya kuwakusanya na kuwaongoza wananchi kufyeka mahali palipokusudiwa kujengwa uwanja huo huko Sebleni.


Katika kuona jambo hilo linafanikiwa, wazee kwa vijana, wanaume kwa wanawake, wakuu wa chama na serikali pamoja na wananchi walishiriki vilivyo katika ufyekaji huo.
Wananchi hao bila ya kujali vyama vyao, mvua wala jua walijumuika pamoja katika kusafisha eneo hilo ambalo limetumika kwa ujenzi wa uwanja wa Amaan, na hadi sasa wananchi wa visiwa wananeemeka na uwanja huo.


Eneo la ekari 22 lilipatikana mapema kuliko ilivyotarajiwa ambapo wananchi mbali mbali wakiongozwa na marehemu mzee Abeid Karume walianza matayarisho ya uwanja.
Mnamo Novemba 1969, ujenzi wa uwanja ulipamba moto pamoja na mnamo Januari 12 , 1970, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere, aliufungua uwanja huo uliopewa jina la ‘AMAAN’.


Mara baada ya kumalizika kujengwa uwanja huo, pambano la kwanza lilifanyika baina ya Young African na timu mchanganyiko ya Elimu na Wanamaji wa Zanzibar, mchezo huo ulikuwa mkali na kusisimua ambapo miamba hiyo ilitoka sare.


Ujenzi wa uwanja huo wa kisasa pamoja na hoteli ya uwanja wa kwa ujumla wake ikiwemo vifaa vyake vyote viligharimu shilingi za Kitanzania milioni 6,000,000 .
Lakini uwanja huo mkubwa ambao umetimia vipimo vyote, pia pembezoni mwake vipo viwanja vidogo vidogo kwa ajili ya mazoezi, lakini, hivi sasa pia vinatumika kuchezewa mechi za madaraja mbali mbali ikiwemo pia vijana.


Kwa hakika ni faraja kubwa kwa wananchi wa Zanzibar kuwa na uwanja huu kisasa ambao hadi leo unaendelea kuwa wenye hadhi ya kimataifa, ambapo michezo mbali mbali ya kimataifa huchezwa.


Mbali na huo wa zamani ambao marehemu Mzee Karume aliusimamia kwa nguvu zote, pia uwanja wa Gombani ni miongoni mwa viwanja ambavyo vina hadhi ya kimataifa.
Mbali na uwanja huo wa Amaan pia Zanzibar ilipata nafasi nyingi muhimu ya kuwa na uwanja wa mpira wa miguu wa Mao Zedong, amabo nao umeleta faraja nyingine kwa wanamichezo baada ya serikali ya China kuamua kujenga upya uwanja huo.


Uwanja wa Mao Zedong hivi sasa serikali hii ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na Serikali ya watu wa China, zimeamua kuufanyia matengenezo makubwa na kuurejeshea hadhi yake, kwani ni moja ya viwanja ambavyo vimebeba historia kubwa ya visiwani pamoja na nchi ya China.


Historia inaonyesha kuwa mashindano ya kwanza ya Afrika Mashariki ‘ Kombe la Goseji, ambayo hivi sasa yanajulikana kwa jina la Chalenji yalifanyika kwenye uwanja huo mwaka 1949, wakati huo uwanja huo ukijulikana kwa jina la ‘Seyyid Khalifa Sports Ground’.
Hata hivyo kutoka mwaka 1947 – 1966 Zanzibar ilikuwa ikishiriki mashindano hayo, lakini, haikuwahi kupata ushindi, licha ya kucheza kwa kiwango kizuri bahati haikuwa yao.


Mbali na michezo hiyo pia michezo ya riadha ilikuwa ikifanyika ambapo mwaka 1894, mashindano ya mwanzo ya riadha yalifanyika baina ya Wanamaji wa H.M.S ambao walicheza wenyewe kwa wenyewe ambayo yalifanyika katika viwanja vya Coopers hivi sasa vinajulikana kwa jina la viwanja vya Maisara.


Kwa wakati huo licha ya kuwa yalikuwa mashindano makubwa na mazuri, lakini, zaidi waliokuwa wakishiriki mashindano hayo ni wanafunzi wa skuli mbali mbali pamoja na askari polisi.
Mbali na hayo, pia michezo mbali mbali ilionekana kuimarika pamoja na viwanja vyake ikiwemo michezo ya tenisi, mpira wa wavu na gofu kuanzia mwaka 1888, lakini, klabu ambazo zilikuwa zikishiriki ni zile za kikabila na zaidi walikuwa wakitumia viwanja vyao kwenye maeneo mbali mbali.
Mbali na viwanja hivyo vya mpira wa miguu pia vipo viwanja vyengine ambavyo ni maarufu vinavyojulikana kwa viwanja vya kufurahishia watoto, ambavyo vipo Tibirinzi Pemba na Kariakoo Unguja.


Mawazo ya kutaka kuanzishwa ujenzi wa viwanja hivyo yalitolewa na Hayati Mzee Abedi Karume, kwa nia ya kuwafanya watoto kusherehekea vyema wakati wa sikukuu mbali mbali zinapokuwepo.
Uwanja wa Tibirinzi ulianza kujengwa mwaka 1972 wakati huo mzee Karume alishafariki dunia,lakini, hatua za awali za ujenzi huo alizianzisha ambapo viwanja hivyo viliwekewa pembea za kisasa na kuwafanya watoto kusherehekea kwa amani na furaha tele.


Hongera Dk. Shein kwa mafanikio ya uongozi wako wa miaka 10 na kuendeleza kwa vitendo fikra, mawazo na imani thabiti ya Marehemu Mzee Abeid Amani Karume.