NA MASANJA MABULA, PEMBA
MAKOSA mawili ya kutorosha na kubaka, yamemsababishia kijana Talib Rashid Sinani wa kizimbani Wete, kupelekwa Chuo cha Mafunzo kwa kipindi cha miaka minne, adhabu iliyotolewa na mahakama ya Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Kijana huyo mwenye umri wa miaka 18, alitenda kosa hilo baina ya Disemba 7 na 15 mwaka huu majira ya saa 10:00 za jioni, makosa ambayo alimfanyia msichana mwenye umri wa miaka 16.
Kosa la kutorosha ni kinyume na kifungu cha 113 (1) (a) cha sheria ya adhabu namba 6/2018 sheria za Zanzibar.
Aidha kwa kosa la kubaka ni kinyume na vifungu vya 108 (1) (2) (e) na 109 (1) vya sheria ya adhabu namba 6/2018 sheria ya Zanzibar.
Kesi hiyo ilifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Machi 4, 2019 ambapo jumla ya mashahidi wanne walitoa ushahidi wao na hukumu kutolea hapo jana.
Kabla ya adhabu hiyo, Mwendesha Mashtaka wa Serikali Juma Mussa Omar, aliiomba mahakama itoe adhabu kali kwa mtuhumiwa huyo ili fundisho kwa wengine wenye tabia kama hiyo.
“Naomba mahakama yako itoe adhabu kali kwa mtuhumiwa, kwani matendo kama haya yamekithiri ndani ya jamii, ili iwe fundisho kwa wenye tabia kama hii”, alisema.