NA LAYLAT KHALFAN
NI siku chache tu tangu ofisi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma ya Maji na Nishati Zanzibar (ZURA) kutiliana saini kwa kazi ya ujenzi wa mradi wa uhuishaji na uimarishaji wa mfumo wa usambazaji maji Zanzibar.
Mradi huu unaotekelezwa kwa mkopo wa dola za kimarekani milioni 92.18 kutoka Exim Bank India, pamoja na mambo mengine lakini mradi huu umelenga kuondoa tatizo la maji safi na salama katika shehia za Kama, Mfenesini, Mwakaje, Bumbwisudi, Mbuzini, Chuini, Kihinani, Dole, Kizimbani, Bububu, Mwanyanya, Kibweni na Sharifumsa.
Aidha mradi huo utawafaidisha maeneo ya Masingini, Mtofaani, Kianga, Mwera, Ubago, Jumbi, Tunguu, Fuoni, Kibondeni, Fuoni kijitoupele, Pangawe, Kinuni, Magogoni, Mwanakwerekwe, Meli nne na Tomondo.
Halkadhalika maeneo ya Maungani, Kisauni, Shakani, Nyamanzi, Kombeni, Dimani, Bweleo na Fumba nazo zitafaidika katika mpango huo.
Kwa kuwa maji ni ‘uhai kwa viumbe hai’ hivyo kuweko kwa mpango huo utasaidia sana Wananchi ambao kwa miaka kadhaa walikuwa hawafaidiki na huduma hiyo.
Tunaipongeza Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) kwa kuwajali wananchi katika kuwasogezea huduma hii kwani bila ya maji hakuna kinachokuwa hasa katika kujiletea maendeleo ya mtu mmojammoja na taifa kwa ujumla.
Ukiachilia mbali shehia zilizotajwa ZAWA hivi sasa wapo katika mazungumzo na mradi wa ADB mpya ambao unakusudia kupeleka huduma ya maji kwa kisiwa cha Uzi na Uzing’ambwa ili kuondosha tatizo hilo lililosumbua muda mrefu wakaazi wa maeneo hayo.
Kwa mnasaba huo, wananchi walengwa wa mradi husika, wawe tayari kuupokea maradi huo na hasa pale ambapo maji yatakapotoka kuchangia huduma hiyo ili ZAWA ipate nguvu ya kununua vifaa na huduma iwe endelevu kwa maeneo mengine ambayo haijafika huduma hiyo.
Kama inavyoeleweka ZAWA pamoja na huduma ya uungaji wa maji lakini pia ianahitaji kupewa ushirikiano wa karibu hasa pale ynapopasuka mabomba wananchi kuripoti sehemu husika na kufanyiwa matengenezo haraka.
Mradi huu utatekelezwa katika kipindi cha miezi 18 kuanzia Agosti 2020 na mara baada ya kukamilika kwake utanufaisha wakaazi wote wa shehia zilizotajwa katika upatikanaji wa huduma bora ya maji safi na salama .
Ni imani yangu kwamba utekelezaji wa mradi huu pamoja na miradi mingine iliyotangulia ni ishara ya maendeleo makubwa katika sekta ya maji nchini, hivyo tunawataka wananchi na watumiaji wa maji hapa nchini, kuihami na kuitunza miradi kama hii kwa kulipia huduma ya maji ili iwe endelevu kwa jamii ya sasa na vizazi vijavyo.
Mradi huu ni ni miongoni mwa jitihada za serikali ya awamu ya saba ya Mapinduzi ya Zanzibar lakini pia ni utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa wananchi wa Zanzibar.