NA MWANAJUMA MMANGA

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imesema imeanzisha taasisi za utafiti katika Wizara mbali mbali ikiwemo ya Kilimo kwa lengo la kuzisaidia Wizara kuongeza tija na ufanisi katika kazi zao.

Waziri wa Kilimo Maliasili Mifugo na Uvuvi, Mmanga Mjengo Mjawiri aliyasema hayo wakati akizindua bodi za Wakurugenzi za wizara hiyo huko Ukumbi wa ASSP Maruhubi.

Alisema hatua hiyo itasaidia sekta ya kilimo katika kujua matatizo yanayowakabali wakulima, wavuvi na wafugaji kutokana na utafiti utaofanywa, kwani hivi sasa wakulima waliowengi wamekuwa na kipato cha chini, hivyo kuwepo kwa bodi hizo kutawawezesha wakulima hao kujua mbinu zitakazowaongezea kipato, ili kujikwamua kiuchumi.

Aidha Mjawiri amezitaka taasisi hizo kubuni mbinu ambazo zitawawezesha kupata fedha za kuwaendeshea katika tafiti zao na kufikia malengo yaliokusudiwa.

“Matumaini yangu kwamba bodi hii itakuwa ni moja ya chombo ambacho kitaweza kutatua changamoto mbali mbali za sekta ya kilimo, ili kufanya kilimo kiwemo bora na kuleta tija kwa sekta hiyo sambamba na kuongeza uzalishaji kwa kilimo” alisisistioza Mmanga.