NA MARYAM HASSAN

NDIZI aina ya Pukusa mkungu mmoja imempandisha katika mahakama ya wilaya Mwera mshitakiwa Talib Mwinyi Ali (33) mkaazi wa Koani.

Mshitakiwa huyo alipanda mahakamani hapo mbele ya Hakimu Rauhia Hassan Bakari, na kusomewa shitaka lake na mwendesha Mashitaka wa Serikali Muzne Mbwana, ambapo alidai kuwa Mshitakiwa alitenda kosa hilo Januari 2, mwaka jana majira ya saa 3:15 za asubuhi huko Koani wilaya ya Kati mkoa wa Kusini Unguja.

Alidai, bila ya halali na kwa udanganyifu na bila ya kuwa na dai la msingi aliiba ndizi aina ya Pukusa mkungu mmoja ikiwa na thamani ya shilingi 7000, mali ya Masoud Mohammed Bakari, jambo ambalo ni kosa kisheria.

Aliposomewa shitaka lake mshitakiwa huyo alikataa na kuiomba mahakama kumpa dhamana jambo ambalo lilikubaliwa mahakamani hapo.

Kwa upande wa wakili wa serikali alisema kwamba upalelezi wa shauri hilo umekamilika na kuomba kuahirishwa shauri hilo na kupangwa tarehe nyengine kwa ajili ya kusikilizwa mashahidi.

Kwa upande wa Hakimu wa mahakama hiyo alimtaka mshitakiwa kujindhamini mwenye bondi ya shilingi 50,000 pamoja na wadhamini wawili ambao watasaini kima hicho hicho na kuwasilisha kopi ya kitambulisho cha Mzanzibar mkaazi pamoja na barua ya Sheha.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Seotemba 2, kwa kuanza kusikilizwa mashahidi.