WASHINGTON,MAREKANI

MKUTANO  mkuu wa chama cha Demokratik cha Marekani, ambapo uteuzi rasmi wa mgombea urais pamoja na mgombea mwenza utafanyika, ulianza jana katika mji wa Milwaukee,na utaendelea kwa siku nne.

Aliyekuwa Makamu wa Rais wa Marekani Joe Biden na Seneta anayewakilisha jimbo la California, Kamala Harris, wanatarajiwa kukubali rasmi uteuzi wa chama chao, kama Mgombea urais na mgombea mwenza .

Pamoja na wao kukubali uteuzi huo, hafla mbalimbali zimepangwa kufanyika katika siku hizo nne, na viongozi wa ngazi ya juu kwenye chama hicho, wakiwa ni pamoja na Rais wa zamani wa Marekani, Barack Obama, kutoa hotuba zao.

Wanasiasa John Kerry, Alexandria Ocasio-Cortez pia watahutubia wafuasi wao kwa njia ya mtandao.

Ingawa kwa kawaida mikutano mikuu ya vyama huvutia maelfu ya watu, mwaka huu hali ni tofauti na wafuasi wengi wa chama hicho wanatarajiwa kufuatilia kupitia vyombo vya habari.

“Mkutano wa mwaka huu utakuwa na utofauti mkubwa mno na mikutano ya miaka iliyopita kwa sababu unafanyika katika mazingira ya janga la Corona, hali ambayo haijawahi kushuhudiwa tena katika historia ya Marekani,” alisema Dkt Patrick Nighula, Mhadhiri wa chuo kikuu cha South Carolina,

Ikulu ilikubali kwamba Seneta Kamala Harris anaweza kuwa makamu Rais, na kumaliza tetesi zilizokuwa zikirudiwa na Rais Donald Trump kwamba mwanasiasa huyo alikuwa hastahili kuhudumu wadhifa huo.

Harris alizaliwa nchini Marekani na wazazi wahamiaji na RaisTrump amekuwa akikosolewa kwa kutochukua msimamo wa wazi kuhusu tetesi hizo.

Mkutano mkuu wa chama cha Republikan utaanza Agosti 24 na kuendelea hadi Agosti 28 ambapo Rais Donald Trump pamoja na makamu wake, Mike Pence, wanatarajiwa kukubali uteuzi wa chama chao wa kugombea urais kwa muhula wa pili.