BEIRUT,LEBANON

MKUU  wa mamlaka ya forodha ya Lebanon alikamatwa, baada ya kuhojiwa juu ya mripuko mkubwa mjini Beirut mapema mwezi huu.

Uchunguzi dhidi ya maofisa wanaokamatwa, unalenga kufahamu kwanini tani 3,000 za kemikali ya amoniamu nitrate zilikuwa zimehifadhiwa kwenye bandari.

Shehena ya kemikali hiyo ndio ilisababisha mripuko uliowaua watu zaidi ya 170 na kujeruhi wengine 6,000.

Watu 30 bado hawajapatikana baada ya mripuko wa Agosti 4 uliosababisha uharibifu wa karibu dola bilioni 15.

Zaidi ya watu 70,000 wanaaminika kukosa ajira kutokana na mkasa huo.

Rais wa Lebanon Michel Aoun alisema uchunguzi juu ya janga hilo ni mgumu na hautokamilika haraka.

Naye msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric aliongeza kuwa watu wapatao 220,000 wanakadiriwa kupoteza kazi zao kutokana na mgogoro wa kifedha ulioanza Oktoba mwaka uliopita.