ZASPOTI
MSIMU wa Ligi Kuu ya Zanzibar mwaka 2019/20 umemalizika kwa Mlandege kutwaa ubingwa baada ya kuukosa kwa karibu miaka 22, ikijikusanyia pointi 68 miongoni mwa klabu 16 zilizoshiriki ligi hiyo.

Mlandege ambayo ilianzishwa mwaka 1970, ilianzia ligi za soka za madaraja ya vijana ambapo mara ya mwisho kuchukuwa ubingwa huo ilikuwa mwaka 1998 kabla ya kupotea kwenye ramani mnamo miaka 2000 kutokana na kuyumba kiuchumi na kurudi tena mwaka 2016.

Miamba hiyo ilirudi tena mwaka 2016 na kuanza kushiriki ligi daraja la pili wilaya ya Mjini na kutwaa ubingwa chini ya kocha Khamis Gullit ambapo mwaka 2017 ilishiriki daraja la pili Taifa na baadae ilinunua daraja kucheza ligi daraja la kwanza kanda ya Unguja mwaka 2018 na kufanikiwa kupanda hadi ligi kuu mwaka 2019 na kutwaa ubingwa huo wa Zanzibar.

Ubingwa huo umeandika historia kwa timu za uraiani ambapo kwa muda mrefu zilikosa kubeba taji hilo kwa zaidi ya miaka mitano.
Mlandege katika ligi hiyo ilicheza mechi 30, ambapo kati ya mechi hizo ilifungwa mechi mbili, ilitoka sare mechi nane na kushinda michezo 20 na ilichukuwa ubingwa huo chini ya kocha wao Abdulhamid Rashid Juma.

Wakati miamba hiyo ikitwaa ubingwa wa Zanzibar mwaka 1998 na kushiriki michuano ya Afrika ilikuwa chini ya kocha, Hafidh Badru ambapo haikufanya vizuri, lakini, ikawika katika mashindano ya Afrika Mashariki na Kati na kufikia hatua ya fainali dhidi ya timu ya Rayon ya Rwanda, mchezo ambao ulichezwa kwenye uwanja wa Amaan.

Akizungumza na mwandishi wa makala haya, Rais wa Mlandege, Mbaraka Himid, alisema walistahili kupata ubingwa huo kutokana na ushirikiano ulioneshwa baina ya viongozi, wachezaji na wapenzi na wanachama wa timu hiyo.

MAFANIKIO

Alisema kuwa mafanikio ambayo wanajivunia katika timu yao ni kwamba ndio inayoongoza kwa kutwaa ubingwa ikiwa ni mara saba, ikifuatiwa na KMKM ambayo imechukua mara sita kwa vipindi tofauti.

Aidha, aliyataja mafanikio mengine ya kujivunia ni kwamba imewakilisha makombe makubwa ikiwemo Kombe la Muungano, Klabu Bingwa Afrika na Afrika Mashariki.
Mafanikio mengine ni kuwa timu ambayo imezalisha makocha wakubwa ambao wanafundisha timu mbali mbali hapa nchini.

Miongoni mwa makocha ambao wamezalisha na wamekuwa na mafanikio makubwa katika soka ni pamoja na Ali Bushiri, Ali Bakari Mngazija, Salum Ali ‘Chula’ na kocha Abdulhamid Rashid Juma ambae anaendelea nayo mpaka sasa.
Hata hivyo, anasema, siri kubwa ya mafanikio hayo ni nidhamu, umoja na upendo kuanzia ngazi ya uongozi, wachezaji, wapenzi mpaka mashabiki.

CHANGAMOTO

Mbaraka anasema kila panapo kuwa na mafanikio hapakosi changamoto ambapo wao katika klabu yao wanachangamoto kuu tatu.
Changamoto ya kwanza ni ukosefu wa udhamini ndani ya timu na badala yao wanapata ufadhili kutoka kwa mtu mmoja jambo ambalo alilisemea kuwa ni hatari.

Changamoto nyengine ni timu kukosa uwanja wake na wanatumia uwanja wa kukodi uliopo Mbuyuni mkoa wa Mjini Magharibi uwanja ambao kulingana na mazingira hauna viwango bora vya kukidhi mahitaji yao.
Changamoto ya tatu ni kutokuwa na jengo la uhakika la klabu hiyo na badala yao wanatumia ofisi za kukodi kwa ajili ya kuendeshea shughuli zao.
“Uwanja ambao tunautumia tumekodi na ofisi zetu zipo Vikokotoni ambazo nazo tumekodi”, anasema.

MATARAJIO

Rais huyo anasema, matarajio yao ni kuifikisha timu pale palipoachwa na makocha wa zamani ili kuona kama ilifikia nusu fainali ya ifikie fainali na kutwaa ubingwa katika michuano hiyo.
Hivyo aliwataka wachezaji wao kuzidisha bidii na wasibweteke na hatua waliyofikia ili kuweza kupata mafanikio mazuri zaidi katika kuelekea michuano ya klabu bingwa.

Anasema kuwa timu yao ni kweli imetwaa ubingwa, lakini, usiwafanye wabweteke na kujiona wamefika cha msingi ni kuendelea kusikiliza maelekezo ya waalimu wao nini wanataka katika kuipeleka mbele timu hiyo.

Mlandege ni timu kongwe visiwani hapa ambapo kuna wachezaji wengi walipita na wamekuwa na mafanikio mazuri katika kuendeleza soka visiwani hapa.
Miongoni mwa wachezaji ambao wameitumikia timu hiyo ni pamoja na Haji Mwinyi, Clement Kaabuka, Ramadhan Hamza Kidilu, Deo Lucas, Bure Saleh, Othman China, Alfonce Modest, Sabri Ramadhan China ambae bado anaendelea nayo mpaka sasa.

Wengine ni mfadhili wa timu hiyo Abdulsatar Dawood ambae alicheza nafasi ya mlinda mlango wa timu hiyo ambayo aliitumia vyema enzi zake.
Wachezaji wengine maarufu walioichezea timu hiyo ni marehemu Rifat Said, Rajab Mzee ‘Gari Kubwa’, Victor John Bambo, Juma Bakari Kidishi, Edi Enzi.

Kwa upande wa wachezaji ambao waliipatia ubingwa mwaka 1998 ni Simai Prago, Shem Frank, Babeshi, Mohammed Salum Lumbo, Ramadhan Hamza Kidilu, Mohammed Hamza , Feisal Salum na mlinda mlango wao Salum Ali ‘Chula’.
Kwa upande wa makocha ambao wameifundisha timu hiyo ni pamoja na Hafidh Badru, Shaban Ramadhan, marehemu Hussein Kheri, Mzee Kheir na Jaala ambao waliifundisha katika madaraja tofauti.

Kocha ambae alianza nayo timu hiyo kuifundisha katika daraja la central alikuwa ni Khamis Rajab ambae kwa sasa ameachana kabisa na mpira wa miguu.
Miongoni mwa timu ambazo zilishiriki ligi kuu ya Zanzibar katika msimu wa 2019/2020 ni Zimamoto iliyoshika nafasi ya pili pointi 67, JKU ilishika nafasi ya tatu pointi 65, KMKM ilishika nafasi ya nne pointi 56 na Mafunzo ilishika nafasi ya tano ikiwa na pointi 45.

Nafasi ya sita ilichukuliwa na KVZ wenye pointi 44, Kipanga walishika nafasi ya saba pointi 42 sawa na Polisi ilishika nafasi ya nane wakiwazidi kwa magoli na nafasi ya tisa ilichukuliwa na Chuoni yenye pointi 40 na Malindi wakashika nafasi ya 10 wakiwa na pointi 38.
Jumla ya timu sita zilishuka daraja katika msimu huo wa 2019./2020 ni Machomanne, Jang’ombe Boys, Selem View, Mwenge, Jamhuri na Chipukizi.
Jumla ya magoli 508 yalifungwa kwenye ligi hiyo katika michezo yake 240 iliyochezwa.

Babeshi, Mohammed Salum Lumbo, Ramadhan Hamza Kidilu, Mohammed Hamza , Feisal Salum na mlinda mlango wao Salum Ali ‘Chula’.