NA MWAJUMA JUMA

SHIRIKISHO la Soka Zanzibar (ZFF) limeandaa mchezo maalum kwa ajili ya kukabidhi zawadi kwa bingwa mpya wa ligi Kuu ya Zanzibar 2020/2021.

Mchezo huo utachezwa siku ya Jumamosi ya Agosti 8, utawakutanisha mabingwa wa ligi hiyo Mlandege na timu ya taifa ya Vijana chini ya miaka 20,inayojianda na michuano ya vijana itakayofanyika mkoani Morogoro.

Kaimu Katibu wa Shirikisho hilo Ali Ame Vuai alimwambia mwandishi wa habari hizi kuwa mchezo huo utachezwa katika uwanja wa Mao Zedong saa 10:00 za jioni.

“Kama unavyojua ligi imemalizika na bingwa amejulikana pamoja na timu zilizoshuka lakini bado bingwa hajapewa zawadi, sasa tumeandaa mchezo maalum ambao utachezwa na bingwa tutamkabidhi zawadi yake”, alisema Vuai.

Alisema katika hafla hiyo bingwa atakabidhiwa zawadi yake ya kombe pamoja na pesa taslimu ambazo hakuzitaja.

Alisema pia kutatolewa zawadi mbali mbali ikiwemo za mchezaji bora wa ligi pamoja na mfungaji bora.

Hata hivyo alisema katika mchezo huo fedha za kiingilio zitakazopatikana zitakuwa ni mchango kwa ajili ya timu hiyo ya taifa ya vijana.

Ligi kuu ya Zanzibar ilikuwa ikishirikisha timu 16, ilimalizika mwishoni mwa mwezi uliopita ambapo Mlandege ilitwaa ubingwa kwa kuwa na pointi 68 na timu sita zilishuka daraja zikiwemo tano za Pemba na moja ya Unguja.

Timu hizo zilizoshuka daraja ni Jang’ombe Boys, Machomanne , Jamhuri, Mwenge, Chipukizi na Selem View.