NA ABOUD MAHMOUD

WAWAKILISHI wa Zanzibar kwenye mashindano ya klabu bingwa Afrika, timu ya soka la Mlandege, imesema imejipanga kuhakikisha inafanya vizuri,katika mashindano ya kimataifa

Mkurugenzi wa klabu hiyo ambao ni mabingwa wapya wa soka Zanzibar Ali Dai, alitoa kauli hiyo wakati alipokuwa akizungumza na gazeti hili, huko ofisini kwake Migombani, na kusema kwamba klabu hiyo imejipanga kwenda kushindana na sio kushiriki kwenye mashindano ya klabu bingwa Afrika.

Dai alisema mipango ya klabu hiyo katika kufikia lengo hilo ni kufanya usajili mzuri wa wachezaji ambao watasaidia kutimia malengo yao.

“Tumejipanga kikamilifu kuhakikisha mashindano ya kimataifa tutakayoshiriki tunafanya vizuri, hatimae kuchukua ubingwa,lakini pia tumejipanga katika kombe la Mapinduzi na hata ligi kuu msimu ujao kunyakua tena ubingwa,”alisema.

Mkurugenzi huyo alieleza kwamba wanatarajia kusajili mlinda mlango mmoja,washambuliaji watatu, beki mmoja na kiungo mmoja ambao watashirikiana na waliokuwepo katika kufanikisha klabu hiyo kufanya vizuri zaidi.

Kuhusu udhamini, Dai alisema klabu yake imejipanga kuhakikisha inatafuta mdhamini ambae ataidhamini mashindano mbali mbali ikiwemo ya kitaifa na kimataifa.

Alisema mpaka hivi sasa wapo katika mazungumzo na baadhi ya kampuni kupata udhamini wa timu yao,ambapo alisema udhamini huo utasaidia kuinua timu hiyo pamoja na kufanya vizuri.

“Tayari tumeanza mazungumzo na baadhi ya makampuni kwa lengo la kuidhamini klabu yetu katika mashindano mbali mbali, ikiwemo ligi kuu na hata mashindano ya kimataifa,tuna matumaini tutafanikiwa ili timu yetu iweze kufanya uzuri zaidi,”alifafanua.

Dai amewataka mashabiki wa klabu ya Mlandege kukaa mkao wa kula na kutegemea mambo mazuri, nadni ya timu yao na kusema kuwa timu hiyo itakua nzuri na yenye ushindani .

Aidha Mkurugenzi huyo alisema mashabiki wa Mlandege wategemee matokeo mazuri katika mashindano yote watakayoshiriki .

“Tumejipanga Mlandege kurudisha hadhi ya mchezo wa soka na tunataka kuonesha kwamba timu za uraia zina uwezo wa kuchukua ubingwa na sio za askari peke yake,”alisema.

Mlandege FC mwaka 1996 hadi 1999 ilifanikiwa kutwaa ubingwa wa ligi kuu mfululizo na baadae kurudia tena mwaka 2001 hadi 2003 baada ya mwaka huo imefanikiwa tena msimu huu kutwaa ubingwa huo.