WELLINGTON, NEW ZEALAND

MSHAMBULIAJI  wa kizungu ambaye aliwauwa kwa bunduki waumini 51 kwenye misikiti miwili nchini New Zealand jana amehukumiwa kifungo cha maisha jela na kwa sharti kwamba muda wa kifungo hicho hauwezi kupunguzwa.

Jaji Cameron Mander alisema hukumu hiyo ambayo ndiyo ya juu zaidi na kwanza ya kutolewa nchini New Zealand inalenga kuonesha jinsi matendo ya mshambuliaji huyo Brenton Tarrant yalivyokosa utu na ubinadamu.

Jaji Mander ameongeza kusema kuwa makosa yaliyofanywa na mwanamme huyo raia wa Australia ni ukatili wa kiwango kibaya ambao hata hukumu ya maisha jela haiwezi kufuta hasara na maumivu aliyosababisha.

Katika mashambulizi ya Machi 2019, Tarrant aliwashambulia kwa bunduki za rashasha waumini waliokuwa kwenye ibada katika msikiti wa Al Noor na Linwoood mjini Christchurch.

Kisa hicho kiliutikisa ulimwengu na jamii za watu wa New Zealand ambayo ilifanya mageuzi ya sheria zake na kupiga marufuku umiliki wa bunduki za kivita.