NA MARYAM HASSAN

MAHAKAMA ya mkoa Vuga, imemnyima dhamana mtoto wa miaka 17 aliyedaiwa kumuingilia kimwili mtoto mwenziwe wa kike wa miaka 12.

Hatua hiyo imekuja kufuatia mahakama kukataa ombi la dhamana aliloliwasilisha mtoto huyo mbele ya Hakimu Hussein Makame, mara baada ya kukana kosa hilo.

Hakimu huyo alisema, kwa muda huu mshitakiwa atabakia rumande hadi Agosti 24 mwaka huu, kesi yake itakapofikishwa tena mahakamani hapo kwa ajili ya kuanzwa kusikilizwa mashahidi.

Pamoja na hayo, Hakimu Hussein, pia ameutaka upande wa mashitaka uliokuwa ukisimamiwa na wakili wa serikali, kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Issa Suleiman, kuhakikisha kwamba siku hiyo anakuwepo Afisa Ustawi wa Jamii.

Kabla ya kutolewa maamuzi hayo, Wakili huyo wa serikali aliieleza mahakama kwamba, upelelezi umekamilika juu ya shauri hilo na kuomba lipangiwe tarehe nyengine kwa ajili ya kusikilizwa.

Mshitakiwa wa kesi hiyo ambae ni mkaazi wa Pangawe, amefikishwa mahakamani hapo kwa kosa la kubaka, kitendo ambacho ni kinyume na vifungu vya 108 (1) (2) (e) na 109 (2) vya sheria namba 6 ya mwaka 2018 sheria za Zanzibar.

Ilidaiwa mahakamani hapo kwamba, mshitakiwa huyo alitenda hilo hilo Agosti 3 mwaka huu majira ya saa 9:00 za jioni, huko Pangawe wilaya ya Magharibi ‘B’ mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Siku hiyo anadaiwa kumuingilia kimwili mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 12 ambae si mke wake, jambo ambalo ni kosa kisheria.