NA MARYAM HASSAN

MAHAKAMA ya watoto Vuga, imemtoza faini ya shilingi 200,000 pamoja na fidia ya shilingi 50,000 mtoto wa miume wa miaka 17, aliyepatikana na hatia ya kumtorosha mtoto wa kike wa miaka 17.

Adhabu hiyo imetolewa na Hakimu Nayla Abdulbasit, wakati alipokuwa akisoma hukumu kwa mshitakiwa huyo, aliyekuwa akikabiliwa na mashitaka mawili ya kutorosha na kumkashifu mtoto huyo.

Kwa mujibu wa mahakama hiyo, hadi ifikapo Septemba 7 mwaka huu mshitakiwa huyo awe tayari ameshalipa fedha hizo, endapo akishindwa atatumikia Chuo cha Mafunzo kwa muda wa mwezi mmoja.

Mshitakiwa aliyepewa adhabu hiyo ni mkaazi wa Muyuni ‘C’ wilaya ya Kusini mkoa wa Kusini Unguja, ambae alifikishwa mahakamani hapo kwa kosa la kumtorosha na kumkashifu mtoto mwenziwe wa kike mwenye umri wa miaka 17 (jina linahifadhiwa), aliye chini ya uangalizi wa wazazi wake.

Kabla ya kutolewa maamuzi hayo, Wakili wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Zalha Makame, aliiomba mahakama kutoa adhabu kwa mujibu wa makosa aliyoshitakiwa nayo.

Aidha kwa upande wa mshitakiwa alikuwa akiwakilishwa na Wakili wa utetezi Hafsa Ame, kutoka kampuni ya Uwakili ya Hud Hud.

Wakili huyo aliiomba mahakama kuzingatia kuwa aliyeshitakiwa hapo ni mtoto na hivi sasa anajutia makosa yake.

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, mshitakiwa anadaiwa kutenda kosa hilo Februari 23 mwaka jana majira ya saa 4:00 asubuhi huko Muyuni ‘C’ wilaya ya Kusini mkoa wa Kusini Unguja.

Siku hiyo, alidaiwa kumtorosha mtoto wa kike wa miaka 17 kutoka Muyuni ‘C’ na kumpeleka katika banda lake huko huko Muyuni ‘C’, bila ya ridhaa ya wazazi wake.

Aidha mshitakiwa huyo anadaiwa kumkashifu mtoto huyo kwa kumnyonya mdomo na maziwa bila ya ridhaa yake, jambo ambalo ni kosa kisheria.