LUANDA, ANGOLA

MAHAKAMA kuu ya Angola, imemhukumu kwenda jela miaka mitano Jose Filomeno dos Santos, mtoto wa kiume wa rais wa zamani wa nchi hiyo yenye utajiri wa mafuta, kwa udanganyifu wakati alipoongoza mfuko wa taifa wa utajiri wa nchi hiyo.

Dos Santos mwenye umri wa miaka 42, aliitwa mbele ya mahakama Disemba mwaka jana kuhusiana na madai ya ubadhirifu wa dola bilioni 1.5 kutoka katika mfuko huo wa utajiri wa taifa, ambao alikuwa akiuongoza kuanzia mwaka 2013 hadi 2018.

Akiwa na jina la utani la Zenu, Dos Santos alishitakiwa kwa kuiba dola milioni 500 kutoka katika mfuko huo na kuhamisha fedha hizo kwenda katika benki ya Uswisi.

Washitakiwa wenzake watatu, ikiwa ni pamoja na gavana wa zamani wa benki ya taifa ya Angola BNA Valter Filipe da Silva, wamehukumiwa kati ya miaka minne na sita jela kwa wizi wa udanganyifu, ubadhirifu wa fedha na kutumia ushawishi.