NA MWAJUMA JUMA

TIMU ya mpira wa Kikapu ya Sixers imeanza vyema ligi B kwa kuifunga Muembetanga pointi 70-54.

Mchezo huo ambao ni wa ufunguzi ulichezwa kwenye uwanja wa Mao Zedong saa 11:00 alaasiri na kuonesha upinzani mkali.

Katika mchezo huo miamba hiyo ilionesha dalili za ushindi mapema baada ya kuimaliza robo ya kwanza wakiwa wanaongoza kwa pointi 19-6.

Robo ya pili ilianza na miamba hiyo kuendelea kushambuliana na kufanikiwa kwenda mapumziko wakiwa sixers wakiongoza tena kwa pointi 27-15.

Timu hizo zililianza robo ya tatu na katika robo hiyo kulikuwa na ushindani mkali na kumalizika kwa sixers kuvuna pointi 16 na wapinzani wao Muembetanga wakapata pointi 15.

Katika mchezo huo Sixers licha ya kushinda ilizidiwa katika robo ya nne ambayo ilimalizika kwa timu ya Muembetanga kuongoza kwa pointi 18-17.

Wachezaji ambao walikuwa wafungaji bora katika mchezo huo kwa upande wa Sixers walikuwa ni Simon Sprian ambae aliibuka na pointi 21 akifuatiwa na Nassir Abdalla ambae alipata pointi 19.

Kwa upande wa timu ya Muembetanga mchezaji ambae alipata pointi nyingi ni Abdalla Matolla ambae aliondoka na pointi 20.