NA MARYAM HASSAN

MUFTI Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Saleh Omar Kabi, amewataka viongozi wa dini na Serikali kuendeleza utamaduni wa kunawa mikono mara kwa mara, ili kujikinga na maradhi mbali mbali.

Ushauri huo ameutoa huko ofisini kwake Mazizini wakati akifungua mafunzo ya siku moja kwa viongozi hao, kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na ni vyema utamaduni huo ukawa endelevu kwa sababu bado, jamii inakabiliwa na maradhi mbali mbali ikiwemo Corona.

Alisema kitendo kinachofanywa na Wizara ya Afya cha kutoa elimu ya kunawa mikono katika taasisi mbali mbali ni jambo jema linafaa kuzingatiwa kwani kila kiungo cha mwanadamu kinahitaji kukingwa na maradhi mbali mbali yaliopo nchini.

Mapema Katibu wa Mufti, Sheikh Khatibu Ali Mfaume, alisema bado maradhi ya Corona yanaendelea kutesa ulimwenguni na kupelekea vifo na aliwataka viongozi hao kuchukua elimu hiyo na kuendelea kuisambaza, ili wananchi waendelee kujikinga na maradhi hayo.

Issa Abeid Mussa mtoa mada katika semina hiyo alisema Shirika la Afya Duniani (WHO), limeandaa kongamano maalum juu ya unawaji wa mikono ambalo linatarajiwa kufanyika Oktoba 15 mwaka huu, kwani utafiti unaonesha kuwa sehemu nyingi hapa Zanzibar haziwekwi vitakasa mikono baada ya serikali kuregeza masharti ya Corona.

Pia alisema tayari dunia nyengine maradhi ya Corona yamezuka kwa mara ya pili kwa sababu ya kudharau masharti yaliyowekwa na wizara husika.

Wakichangia mada hiyo mmoja wa washiriki hao, Sheikh Mziwanda Mohammed, alisema imefika wakati kwa jamii kutambua kuwa bado nchi ipo katika hali ya mpito juu ya maradhi ya Corona na tahadhari inahitajika.

“Khofu yangu ni kuwa maradhi haya yakijazuka tena sijui tutayakabili vipi kwa sababu tunaonekana kuwa tumepuuza kabisa tahadhiri zote, Allah atukinge” alisema Mziwanda.