Upole wake sawa na simba mwenda kimya
NA MWANDISHI WETU
VISIWA vya Zanzibar na Jamhuri nzima ya Muungano wa Tanzania, kipindi hiki ziko katika vuguvugu kubwa la kisiasa.
Vuguvugu hilo linatokana na matakwa ya kikatiba yanayolipeleka taifa hilo katika uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Jumatano ya Oktoba 28, 2020.
Hiyo itakuwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania kuendesha uchaguzi wake mkuu katikati ya wiki ambayo kwa kawaida ni siku ya kazi.
Tayari mamlaka kuu imeshatangaza kwamba siku hiyo itakuwa mapumziko ili kuwapa nafasi Watanzania wenye sifa ya kupiga kura kutumia haki yao hiyo ya kikatiba.
Uchaguzi huo utahusisha nafasi za maraisi wawili, wa Jamhuri ya Muungano na wa Zanzibar.
Baada ya kufanyika kwa uchaguzi huo, Serikali ya Mapinduzi Zanzinar itakuwa inaingia katika awamu ya nane ya uongozi tangu ilipojikomboa kufuatia Mapinduzi matukufu ya Januari 12, 1964 chini ya muasisi wake marehemu Abeid Amani Karume.
Huku wagombea wa nafasi za urais kwa upande wa Chama cha Mapinduzi wakiwa wameshapatikana, ambao ni Dk. John Pombe Magufuli kwa upande wa Tanzania na Dk. Hussein Ali Hassan Mwinyi kwa serikali ya Zanzibar, makala haya yanajikita katika kuelezea hisia na matumaini ya Wazanzibari hasa wanachama wa CCM kwa Dkt. Mwinyi.
Kama tujuavyo, Tanzania sasa iko katika mfumo wa vyama vingi vya kisiasa ambapo uchaguzi hutawaliwa na ushindani kwa kila chama kuwania kushika dola na kuvuna wingi wa viti katika vyombo vya kutunga sheria, bunge (Tanzania) na Baraza la Wawakilishi (Zanzibar).
Iwapo mwaka huu CCM itafanikiwa kuendeleza ushindi wake wa kila uchaguzi kwa pande zote za Jamhuri, ni wazi Dkt. Husein Mwinyi atakuwa Rais wa kwanza kuongoza Zanzibar ambaye hakuyaona Mapinduzi ya 1964.
Marais wote waliopita, walizaliwa kabla ya Mapinduzi hayo na wakati yakifanyika, tayari walikuwa na akili timamu na uelewa wa kutosha.
Katika umri wake wa miaka 54 aliyonayo sasa, mteule huyo anatarajiwa kuja na nguvu mpya itakayomuwezesha kusimamia vyema mikakati ya kuipaisha Zanzibar kimaendeleo, akiendeleza pale atakapoachia mtangulizi wake, Dkt. Ali Mohamed Shein.
Hata hivyo, mwandishi wa makala haya amesikia baadhi ya watu wa makundi mbalimbali wakionesha wasiwasi wao juu ya ukimya na upole wa mgombea huyo, wakisema huenda akishinda asije na kasi ya nguvu katika kupambana na changamoto za kiuongozi.
Kwa muktadha huo, mwandishi wetu alifanya mahojiano na wananchi mbalimbali ili kujua mitazamo na matumaini waliyonayo kwa daktari huyu wa kutibu binadamu, fani aliyoisomea.
Mwanachama wa CCM na mkaazi wa Miembeni Wilaya ya Mjini ambaye hakutaka kutajwa jina lake, anasema kwa upande wake, hana shaka hata chembe kwamba Dkt. Mwinyi ni chaguo sahihi katika nafasi hiyo kubwa.
Mwanachama huyo aliyewahi kujaribu kugombea uwakilishi katika uchaguzi wa mwaka 2010 lakini akashindwa kwenye mchakato wa kura za maoni, anasema mtu akiwa mkimya haimaanishi kwamba ni mwepesi katika kazi na majukumu anayolazimika kuyafanya.
Aidha, anasema urais au uongozi wa taasisi yoyote ile, ni wadhifa unaohitaji busara, maarifa pamoja na elimu, vitu ambavyo anasema Dkt. Mwinyi amebarikiwa kuwa navyo.
Hata hivyo, alieleza kuwa, pamoja na upole wake, anaamini Dkt. Mwinyi kama Mungu atamjaalia kushinda, hatakubali watu watumie khulka yake ya upole kumchezea sharubu, kwani nafasi anayoigombea itamfanya abebe mabegani matarajio ya wengi.
“Kwangu mimi tabia hii aliyonayo, ninamuona kama simba mwenda pole, ambaye kwa kawaida ndiye alae nyama,” alisema na kuongeza:
“Urais sio upagazi au uchukuzi kwamba mtu anahitaji awe na nguvu za miraba minne kuifanya. Akikabidhiwa jukumu la kuongoza nchi lazima aongozwe na hekima, lakini asiwe na muhali kwa watendaji wanaoonekana kuwa ni kikwazo,” alifafanua.
Mwananchi huyo alikwenda mbali kwa kutoa mfano wa uji wa uwele ambao ukiwa katika bakuli au kikombe, una kawaida ya kuota gamba juu na kuficha moto wake, na mtu akiufakamia kwa pupa lazima utambabua na kumuacha na jeraha mdomoni.
Alifahamisha kuwa, kabla kuteuliwa, kulikuwa na mchakato mrefu uliohusisha watia nia 32, na baada ya utaratibu wa kidemokrasia ulioendeshwa kwa haki na uwazi, Dkt. Mwinyi aliibuka kidedea mbele ya wagombea wenzake wawili ambao pamoja naye walifanikiwa kufikia tatu bora.
Kwa upande mwengine, alisema kinachohitajika ni kwa wana CCM wote kumuunga mkono na kumpa ushirikiano kuanzia sasa hadi mwisho wa safari ili kuhakikisha anakipatia chama chake ushindi wa kishindo katika uchaguzi mkuu Oktoba 28, mwaka huu.
“Naelewa kabla kuteuliwa kulikuwa na washindani wengi na kila mmoja alikuwa na watu nyuma yake, lakini lengo lao wote ni kuipa ushindi CCM, kwa hivyo sasa si wakati wa kuendeleza makundi, tuunganishe nguvu kwani safari ndio kwanza imeanza,” alishauri.
Alieleza kutiwa moyo na kauli ya mgombea huyo wakati wa mapokezi yake Unguja na Pemba, kwamba watu watamuelewa hasa watendaji waliokubuhu kwa rushwa, ubadhirifu wa mali ya umma, wazembe na wasiowajibika.
Mwana CCM huyo alisema dhamira ya mteule huyo kuanza kazi kwa gia hiyo, inaonesha anaelewa wapo watendaji waliokalia viti kwa ajili ya maslahi binafsi, na ahadi yake ya kuanza nao, ni salamu kwao na wengine watakaobahatika kuwemo serikalini.
Kama inavyofahamika, Dkt. Mwinyi aliishi nchini Misri akiwa mtoto mdogo wakati baba yake Mheshimiwa Ali Hassan Mwinyi alipokuwa Balozi wa Tanzania jijini Cairo kuanzia mwaka 1977 hadi 1982.
Miongoni mwa Watanzania waliozungumza na mwandishi wa makala haya ni mtu aliyewahi kumsaidia Dkt. Mwinyi kwa masomo ya ziada (Tuitions) jijini Cairo akiwa mwanafunzi wa skuli ya msingi, ambako mwalimu huyo alikuwa akisoma katika Chuo Kikuu cha Al Azhar.
Bila shaka, Mtanzania huyo mwenye asili ya Zanzibar ambaye pia hakutaka jina lake liandikwe gazetini, anazifahamu vyema tabia za mgombea huyo wa urais kwa kuwa alikuwa karibu sana naye kati ya 1980 na 1982 pamoja na kaka na ndugu zake wengine.
“Hussein ni mtaratibu lakini ni mzungumzaji sana kwa watu waliomzoea. Humuoni sana kuzungumza hadharani, si kwamba anaringa au anadharau, bali hayo ndio maumbile yake, si mtu wa kujitoa,” alianza mazungumzo yetu msomi huyo wa Al Azhar Sharif.
Aidha, alisema takriban watoto wote wa Rais mstaafu mzee Ali Hassan Mwinyi si wenye vishindo, ni wataratibu lakini ni waungwana wenye utu.
Kuhusu uongozi, alisema kuwa Dkt. Hussein anayo taaluma ya utawala ambayo alisomea nchini Marekani, na kwa hivyo, iwapo atashinda hatapata taabu katika kuendesha serikali.
Lakini alisema, ili serikali ipate ufanisi, ni lazima wasaidizi atakaowateua, watendaji wa ngazi mbalimbali serikalini na wananchi wote kwa jumla bila kujali vyama vyao, wampe ushirikiano wa kutosha kwani hakuna dola inayoongozwa na mtu mmoja pekee.
Ili kulinda heshima ya baba yake ambaye aliongoza na kumaliza kipindi chake cha uongozi bila dosari, na kwa malezi aliyopata kwa wazazi wake, mwalimu huyo alisema ana imani kubwa kwamba mteule huyo atajitahdi kuhakikisha hadhi ya walezi wake hao haiingii doa.
Alisema, ingawa kila zama zinakuja na mambo na changamoto zake, lakini kitu muhimu na cha msingi katika uongozi, ni kuweka mbele maslahi ya nchi na wananchi, jambo alilosema lilimuinua sana mzee Mwinyi.
Vivyo hivyo, alieleza kuwa kiongozi hapaswi kulewa madaraka, au kukiona cheo alichonacho ni mali yake binafsi, na hivyo kukitumia ‘kuwakoga’ wengine na kuwaona si lolote si chochote mbele yake.
“Katika hilo na kwa misingi aliyokulia ya maadili, ucha Mungu, heshima na kutodharau mtu wa aina na rika lolote, Dkt. Hussein akipewa dhamana hii kubwa na kwa ushirikiano na wenziwe, Zanzibar itafika mbali kimaendeleo,” alifafanua.
Nilimuuliza mwalimu huyo anaionaje kauli ya mgombea huyo juu ya wala rushwa na watendaji wasiowajibika ipasavyo?
Akijibu suala hilo alikiri kuwa rushwa ni ugonjwa ulioota mizizi katika sekta nyingi za umma na binafsi, na kwamba hatua ya serikali kuunda mamlaka ya kupambana nayo sambamba na uhujumu uchumi, ni kielelezo kuwa tatizo hilo lipo.
Hata hivyo, alisema pamoja na jitihada za ZAECA, bado kasi ya kupambana na rushwa ni ndogo ikikabiliwa na vikwazo kadhaa ikiwemo muhali na hofu ya kukosa kazi pale kunapokuwa na kadhia inayogusa ‘vigogo’.
Alimsifia Dkt. Mwinyi kwa kuliona hilo na kueleza bayana kwamba hatamuonea haya mtendaji yeyote atakaebainika kujihusisha na rushwa, uzembe na ukorofi ili kujenga ustawi mzuri wa nchi na wananchi.
“Ili kutekeleza kwa ufanisi mikakati ya kuinua uchumi na kuimarisha huduma za jamii, lazima fedha za umma zilizopo na zile zinazopatikana ziwe chini ya ulinzi usiopepesa kuhakikisha hakuna senti inayovuja kuingia kwenye mifuko ya watendaji wasiokuwa waaminifu,” alisema.
Alisema, kwa indhari iliyotolewa mapema na Dkt. Mwinyi, akilimudu hilo, ni wazi wananchi watazidisha upendo na imani kwake, na haitashangaza, kuanzia uchaguzi huu na ule wa mwaka 2025 Mungu akijaalia, kuona nguvu ya upinzani ikimeguka na kuiunga mkono CCM.
Baadhi ya wanachama na wapenzi wa vyama kadhaa vya upinzani ambao walikuwa wakifuatilia mchakato wa kupata mgombea wa CCM na mapokezi ya mteule Dkt. Mwinyi, hawakuficha butwaa zao juu ya walichokiona.
Awadh Seif (49) ambaye kwa kauli yake si mshabiki wa siasa ingawa mara zote mbili alizowahi kupiga kura (2010 na 2015) alichagua chama cha upinzani, alisema anaiona turufu ya ushindi kwa CCM katika uchaguzi mkuu ujao.
“Mimi sipendelei sana mambo ya kisiasa lakini sipotezi haki yangu ya kupiga kura. Leo naiona nuru mpya ikiangaza Zanzibar, ambayo inaweza kubadili nyoyo hata za wanachama na wapenzi wapinzani lakini wenye kupenda maendeleo,” alieleza.
Bi. Mwanasiti Uwesu (Sio jina lake halisi), ni mjasiriamali aliyesema mtazamo wake daima ni maendeleo ingawa ni mwanachama wa chama kimoja cha upinzani hapa Zanzibar.
Nilimkuta eneo la Kisiwandui siku ya mapokezi ya Dk. Mwinyi kutokea Dar es Salaam akiwa katika biashara zake nyuma ya Makao Makuu ya CCM.
Nilipomdadisi juu ya hisia zake kwa mgombea huyo, alisema wazi kuwa, kwa mtu mwenye uchungu na nchi yake ambaye hamuabudu kiongozi anayelazimisha awe Rais ndio aone raha ya siasa, hali hiyo ni funzo muhimu la kumfanya abadilishe msimamo.
Alisema ingawa Tanzania iko katika mfumo wa vyama vingi, sio vibaya wanachama wa vyama vyengine wapime upepo ili kama mgombea wa chama kisichokuwa chao anauzika kuliko wa kwao, wampigie kura.
“Vipo vyama ambavyo kila uchaguzi vinashiriki lakini vinang’ang’ania mgombea huyo huyo hata awe mgonjwa aliyelazwa ICU. Ninawashauri kama plani A imeshindwa watumie plani B,” alitoa ya moyoni.
Mama huyo mjane aliyejiajiri kuuza chakula, alisema ishara ziko wazi kwamba kwa mgombea huyu CCM itavikimbia vyama vyengine kwa mbali mno.
Alipoulizwa iwapo Dkt. Mwinyi atashinda, nini changamoto atakayopenda aitafutie dawa chini ya serikali ijayo, Bi. Mwanasiti alisema anataka mazingira huru yenye utulivu kwa wafanyabiashara na wajasiriamali wanawake na vijana ili wafanye kazi kwa ufanisi.
“Mara nyengine tunakumbwa na timua timua za Manispaa ambapo hata bidhaa na vifaa vyetu husombwa na sisi kushtakiwa. Hapa ndio kwetu hatuna pengine. Tupewe nafasi tutafute riziki halali tusilazimishwe kujiingiza kwenye ajira zisizokuwa na staha kama wasichana wengine wanavyofanya,” alianika ndwele inayomuumiza.
Baadhi ya wananchi waliokuwa wakifuatilia kipindi cha ‘Muelekeo Wetu’ katika televisheni ya Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) wiki iliyopita, walipopata nafasi ya kutoa maoni kwa njia ya simu, waliguswa na kauli ya Dkt. Mwinyi aliposema; ‘WATANIELEWA’.
“Mtanielewa katika mapambano dhidi ya rushwa, ubadhirifu, uzembe na kutowajibika,” alikaririwa Dkt. Mwinyi akisema katika njia ya kutuma salamu kwa wanaombeza kwa upole na ukimya wake.
Wapo wanaotaka Zanzibar iwe mpya, yaani kama inapata Rais mpya, basi iko haja ya kuwa na Baraza la Mawaziri jipya sio kwa maana ya sura, bali uwajibikaji uliotukuka na usiotia shaka, na wenye dhamira ya kweli kuwatumikia wananchi.
Hawa wanashauri wakati wa kampeni, akiwa jukwaani, mgombea aseme waziwazi kwamba, kila penye chaka linaloficha uovu na wizi wa mali ya umma, anakwenda kufyeka.
Aidha, katika maoni yao, baadhi ya wananchi walieleza kuwa kinachoitafuna Zanzibar ni muhali ambao umekuwa sumu ya maendeleo kwenye dhamira njema iliyootea ndani ya mtima wa Rais wa sasa anayemaliza kipindi chake.
Wameeleza kuridhishwa na jitihada kubwa za Rais Dkt. Shein, lakini wakadai kuwa anaangushwa na baadhi ya wasaidizi waliomzunguka wanaoangalia zaidi maslahi binafsi.
“Tatizo si Rais, bali shida iko kwa watendaji wake wanaomzunguka,” alisema mtazamaji mmoja akisisitiza haja kwa Rais ajaye kulipatia ufumbuzi tatizo hilo kwa kutowaonea haya wenye mbinu za kujinufaisha kwa rasilimali za umma.
Walisema hawana shaka na Ilani ya CCM ambayo ndiyo inayotumika katika kuendesha nchi, lakini wakashauri kila mmoja awe tayari kusahau yaliyopita katika mchakato wa kutafuta mgombea na kwa pamoja sasa waungane kumuunga mkono Rais ajaye kwa imani na mahaba makubwa.