BEIRUT,LEBANON

MWANACHAMA mmoja wa kundi la Hezbollah amepatikana na hatia ya mauaji ya Waziri mkuu wa zamani wa Lebanon Rafik Hariri, mwaka 2005.

Hukumu hiyo ilitolewa na Mahakama inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa mjini The Hague.

Washitakiwa wengine watatu, ambao pia ni wanachama wa Hezbollah, walifutiwa mashitaka na mahakama hiyo.

Hukumu hiyo inaweza kuzusha mivutano zaidi ya kidini,wakati taifa hilo bado liko katika taharuki ya mripuko wa Agosti 4 uliowaua watu 180.

Jaji David Re wa mahakama hiyo maalumu kwa ajili ya Lebanon alisema Salim Jamil Ayyash alipatikana na hatia ya mashitaka yote matano dhidi yake, ikiwemo kitendo cha ugaidi kwa kutumia mabomu na mauaji ya kukusudia ya Hariri na wengine 21.

Hapakuwa na ushahidi kuwa uongozi wa Hezbollah na Syria walihusika kwenye shambulio hilo.