NA MWANTANGA AME

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba, tangu iliingia madarakani  Novemba 3, mwaka 2010 na ifikipa mwezi Oktoba itakuwa ndio inafikia ukomo wake, kwa vile serikali itaitisha uchaguzi Mkuu.

Uchaguzi huo, utafayika ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Katiba ya Zanzibar, ambayo inataka kila aliyepewa jukumu la kuiongoza nchi anapofikia miaka mitano basi uitishwe uchaguzi Mkuu.

Hadi hivi sasa Chama kinachoongoza nchi hii ni Chama cha Mapinduzi, ambacho kwa kiasi kikubwa kimeweza kudumu kwa miaka mingi tangu yafanyike Mapinduzi ya Zanzibar, Januari 12, 1964.

Leo ni mwezi Septemba ni takriban miaka kumi tokea Novemba 2010, ambapo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein alipata,  kwa mara ya kwanza, imani na ridhaa ya Wazanzibari ya kuwa mkuu wa nchi yao ya Zanzibar, akiwa ni Rais wao.

Aidha, hiki ni kipindi chake cha pili tokea mwaka 2016, baada ya kuchaguliwa na wananchi kufuatia ridhaa ya Chama kilichoongoza nchi hii kwa zaidi ya miaka 40 sasa, ambapo Chama Cha Mapinduzi, kimekaa madarakani

Ukichanganya na kipindi kilichoongozwa na mojawapo ya Chama kiasisi kwa CCM, Chama cha Afro Shirazi, cha kuanzia Januari 12, 1964, vyama hivi vya Ukombozi na Mapinduzi vimeshaongoza nchi kwa uweledi na mafanikio makubwa kwa miaka 56 sasa.

Kuwepo madarakani chama hiki ni sehemu ya kupima uwezo wake wa kuongoza katika njia zinazofaa za kuwatumikia wananchi kwa kila aliyepewa dhamana.

Kutokana na hali hiyo ndio maana chama cha Mapinduzi kimeamua kuweka ilani ya CCM ambayo inakuwa ni muongozo mzuri kwa aliyepewa jukumu la kuiongoza nchi kuutumia kufanya shughuli zake.

Moja ya jambo ambalo limo katika utekelezaji wa ilani hiyo ni suala la Kupambana na Umasikini, ikiwa ni kifungu cha  70 cha Ilani hiyo ambapo kinaelekeza mabo mbali mbali kufanyika ndani ya visiwa vya Unguja na Pemba.

Ndani ya miaka mitano ya mwanzo ya uongozi wa Dk. Shein, umeeleza kwamba, Ili kuongeza nguvu na kasi ya kupambana na umasikini katika kipindi kilichopita (2010-2015), Mfuko wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi umeanzishwa.

Kwa kupitia mfuko huo wananchi wengi hususan vijana, wanawake na wafanyabishara wadogo wadogo wameweza kupatiwa mitaji (mikopo) na kujikwamua kiuchumi.