ZASPOTI
NAHODHA wa timu ya Kahawa Veterani, Mohamed Subeit, amewashauri wachezaji kuendelea kufanya mazoezi kwa bidii ili kurudi katika hali ya ubora wao.
Alikuwa akizungumza na Zaspoti baada ya kumalizika kwa mchezo wa kirafiki dhidi ya Urafiki Veterani katika uwanja wa Urafiki, Kibandamaiti ambapo Kahawa walishinda mabao 3-2.
Alisema hayo baada ya kubaini baadhi ya wachezaji kushuka viwango kutokana na muda mrefu kutofanya mazoezi kufuatia janga la ‘corona’ lililoikumba dunia.
Hata hivyo, alisema, michezo ni ajira kama ajira nyengine,hivyo wanamichezo wanapaswa kulinda na kuimarisha viwango na kuacha kujibweteka ili kulinda vipaji vyao.
“Michezo ni afya, ajira nawashauri wachezaji kufanya bidii kwenye mazoezi ili kuimarisha viwango, lakini pia kuendeleza vipaji walivyokuwa navyo”, alisema.
Alipongeza serikali kwa kuruhusu michezo mengine jambo ambalo litawapa hamasa katika kuhakikisha wanamichezo hao wanaendeleza vipaji ,huku kuendelea kuchukua tahadhari katika kujilinda na maradhi katika viwanja.
Akizungumzia mchezo huo kwa ujumla,alisema, timu zilikuwa na ushindani lakini walipambana na kuwafunga wapinzani wao, sambamba na kuwataka wachezaji kutumia michezo kwa kujenga nidhamu na kudumisha amani katika jamii.