WINDHOEK, NAMIBIA

RAIS wa  Namibia Hage Geingob amekataa kupokea fidia iliyotolewa na Serikali ya Ujerumani kwa ajili ya mauaji ya kimbari yaliyofanywa na taifa hilo la Ulaya wakati wa ukoloni.

Jeshi la Ujerumani liliuwa mamia ya maelfu ya watu wa jamii ya Herero na jamii ya Nama kati ya mwaka 1904 na mwaka 1908, wakati wa ghasia za kupinga ukoloni.

Inadaiwa kuwa asilimia sabini na tano (75%) ya idadi ya watu wa Herero na nusu ya idadi watu wa Nama waliuawa na jeshi la Ujerumani.

Nchi hizo mbili zilianza majadiliano juu ya fidia ya kimbari tangu mwaka 2015 na tayari walikuwa na mazungumzo ya duru nane hadi sasa.

Fidia iliyotolewa na Serikali ya Ujerumani bado haijakubaliwa na Serikali ya Namibia na hakukuwa na maelezo zaidi yaliyotolewa kufafanua uamuzi huo.

Ujerumani ilikubali kuomba radhi lakini ilikataa kufikia makubaliano  kati yao ya kuuguza majeraha waliyoyaacha.

Bado Serikali ya Ujerumani haijatoa msimamo kuhusiana na tangazo hilo la Namibia la kukataa fidia hiyo iliyotolewa na dola hilo la Ulaya lililofanya mauaji ya kimbari nchini Namibia katika kipindi cha ukoloni.