NA HAFSA GOLO

TUME ya Uchaguzi Taifa(NEC) Zanzibar, imeanza kufanya  zoezi la uhakiki wa fomu za kugombea nafasi ya ubunge majimboni kwa vyama vya siasa vilivyojitokeza.

Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi Taifa  Wilaya ya Mjini ,Aziza Tahir Omar, alieleza hayo alipokua akizungumza na gazeti hili ofisini kwake Maisara mjini Unguja, ambapo alisema utekelezaji wa hatua hiyo sio utashi wa watendaji wa tume hiyo bali inasimamia maelekezo ya miongozo ya kisheria na taratibu zilizopo.

Aidha alisema siku rasmini ya kurejesha fomu hizo ni  Agosti jana ambapo zoezi hilo limeanza saa 1:00 asubuhi hadi 12:00 jioni  ambapo  utaenda sambamba na uwekaji wa pingamizi ambao utakuwa ndani ya masaa 24, baada ya mgombea kurejesha fomu.

Hivyo aliwataka wagombea na vyama vya siasa vitakavyokuwa na malalamiko dhidi ya wachukuaji fomu hao kuhakikisha wanafata taratibu, ili kuondosha vikwazo visivyo vya lazima hasa ikizingatiwa tume ipo huru na inasimamia sheria na sio matakwa ya mtu binafsi.

“Kasoro zilizojitokeza katika baadhi ya fomu za wagombea zilikuwa ni za kawaida tu “,alisema.

Nae Msimamizi Msaidi kutoka Magharibi “A”, Mzee Mkongea Ali, alisema wachukuaji fomu za ugombea nafasi ya ubunge katika vyama 14 vilivyojitokeza wote wamefanya zoezi la uhakiki wa fomu zao.

Alisema kufuatia hamasa na muitikio wa wachukuaji fomu hizo uliokuwa pamoja na utekelezaji wa miongozo na taratibu za tume wilayani humo, jambo ambalo limesaidia urahisishaji wa majukumu ya kazi zao.