NA MADINA ISSA

MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya, umesema kwa sasa umeweza kuja na huduma za umoja wa afya kwa vikundi mbalimbali ikiwemo wakulima, ili kuweza kuwapatia huduma bora.

Meneja wa Mfuko huo Zanzibar, Ismail Nuhu Kangeta, aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na Zanzibar Leo, katika maonesho ya tatu ya wakulima ya nane nane yanayoendelea katika viwanja vya Dole wilaya ya Magharibi “A’ Unguja.

Alisema kuweka kwa huduma hiyo itasaidia kuwawezesha wananchi hasa kundi la wakulima kujiunga na mfuko huo, kwani wakulima watashajihika na kujiunga katika mfuko itapelekea kupata wanachama wengi.

Alisema, lengo la kujumuika katika kiwanja hicho ni kuwaunga mkono wakulima sambamba na kutoa elimu inayohusu afya kwa wananchi wanaofika katikamaonyesho hayo, ili kujua huduma wanazozitoa katika mfuko huo.

Akizungumzia kuhusu vifurushi vilivyokuwepo katika mfuko huo, alisema kuwa kwa sasa wamekuwa kwa aina tatu ikiwemo najali, kuwekeza na timiza.

“Vifurushi hivi mtu anachagua kulingana na mahitaji yake na bajeti yake ambapo gharama inategemea na kifurushi unachokitaka mwenyewe na familia yake” alisema.

Nao wananchi waliofika katika banda hilo, walisema wamefurahishwa na elimu waliopatiwa na watendaji wa mfuko huo, na kuahidi kujiunga ili kuweza kuendana na wakati juu ya upatikanaji wa huduma za afya sambamba na kuondokana na maradhi mbali mbali ambayo mara nyingi wamekuwa hawendi katika vituo vya afya kwa kuhofia kutoleshwa fedha hasa binafsi.

Mmoja wa wananchi, Hidaya Ali, alisema elimu ameipata ya kutosha jinsi ya huduma zinazotolewa na mfuko huo kwani itasaidia kupata matibabu katika hospitali zilizosajiliwa na mfuko huo.

“Mfuko huu umelenga kutusaidia kwani elimu wanayoitoa wametupa moyo ya kujiunga ambapo pia tumeweza kuona hospitali nyingi zilizosajiliwa na mfuko hivyo hatuna budi kujinga ili kuweza kutusaidia katika upatikanaji wa huduma za matibabu nchini” alisema.