KILA mtu huvutiwa kuwa na mwenza kwa sifa azipendazo, kwa mfano wapo wanaopenda wanawake wanene, wapo wanaowapenda wembamba, wapo wanaume wanaopenda wanawake maarufu, warembo na kadhalika.

Jina la Kim Kardashian ni maarufu sana nchini Marekani na duniani kwa ujumla, amekuwa maarufu kwa sababu nyingi ikiwemo kufanyashughuli za mitindo, vipindi kwenye televisheni, pia amekuwa majasirimali.

Mwanadada huyo amekuwa na vituko vingi ambavyo vimempa umaarufu, lakini katika makala haya si siku yake kuvielezea vituko kadhaa wa kadhaa katika maisha yake.

Mume wa Kim Kardashian ni mmoja kati ya wanamuziki mashuhuri sana nchini Marekani na duniani kwa ujumla, ambaye anaitwa Kanye West, hata hivyo kilichoshitua watu ni kwamba mume huyo amekuwa akijigamba, kujinasibu na kusifia utajiri wa mkewe.

Kwa hakika hili limewashangaza watu wengi duniani kiasi cha kujiuliza je ni sahihi mume kuringa ama kupita kujigamba kwa utajiri wa mkewe?

Hebu kwanza tuangalie utajiri wa Kim Kardashian kwa mujibu wa jarida la Forbes, ambalo limeeleza kuwa Kim Kardashian sio bilionea, lakini hilo halimzuii mumewe ambaye ni mwanamuziki maarufu Kanye West kumpigia debe.

Kiukweli Kim Kardashian si mtu wa kwanza katika familia yake kuhusishwa na ubilionea, mdogo wake Kylie Jenner, aliwekwa kwenye orodha ya mabilionea ya Forbes na baadaye kutolewa kwa madai ya kutoa taarifa za uongo.

Kim Kardashian ambaye ana umri wa miaka 39, ana utajiri wenye thamani ya takribani dola milioni 900 baada ya kuingia mkataba na kampuni ya Coty Inc. kuuza asilimia 20 ya kampuni yake inayouza vipodozi, urembo na manukato kwa kiasi cha dola milioni 200 kwa mujibu wa Forbes.

Kampuni ya urembo ya Kim Kardashian, KKW, iliripotiwa kuwa na thamani ya dola bilioni moja na hivyo kumfanya Kanye West kujitamba kuhusu kiwango cha utajiri wa mkewe, lakini kwa mujibu wa ripoti mpya kutoka Forbes, Kim ana utajiri wa thamani ya dola milioni 900 peke yake.

Mwaka 2019, Kylie Jenner alitajwa kuwa bilionea mwenye umri mdogo zaidi duniani, kwa mujibu wa orodha ya mabilionea ya gazeti la Forbes.

Kylie ambaye ndiye mdogo zaidi katika familia ya Kardashian alielezewa kuwa amepata utajiri wake kutokana na biashara ya vipodozi.

Lakini mwishoni mwa mwezi Machi mwaka huu, jarida hilo hilo la Forbes lilimuondoa nyota wa kipindi cha TV na mfanyabiashara Kylie Jenner katika orodha ya mabilionea na kushutumu familia yake kupandisha thamani ya biashara yake ya vipodozi.

Jarida la Forbes lilisema kuwa familia yake ilikwenda mbali zaidi kwa kumuwakilisha kuwa ni tajiri mdogo, taarifa zikiwa ni tofauti na uhalisia wenyewe.

Forbes ilisema mhasibu wa familia alitoa ushuru na kuonekana kwamba kampuni hiyo ilikuwa imetengeneza mauzo ya zaidi ya dola milioni 300 mwaka 2016 na kudaiwa kuwa mauzo ya mwaka uliofuata yalikuwa dola milioni 330.

Lakini taarifa kutoka kwa kampuni ya Coty, ambazo zinaenea sana zinaonesha kuwa “kampuni ya Jenner ni ndogo na iso na mafanikio makubwa tofauti na ambacho kimekuwa kikisemwa na familia yake kwenye vyombo vya habari ikiwemo jarida la Forbes, kile ambacho inataka wao waamini”, jarida la Forbes limesema.

Taarifa za kampuni ya Coty kwa wawekezaji kuhusu biashara ilionesha kwamba kampuni hiyo ilikuwa na mauzo ya dola milioni 125 pekee kwa 2018.

“Kama vipodozi vya Kylie vilikuwa na mauzo ya dola milioni 125 mwaka 2018, inawezekanaje kwamba ilikuwa na mauzo ya dola milioni 307 kwa mwaka 2016 au dola milioni 330 mwaka 2017?” Forbes ilihoji katika makala hiyo.

Pamoja na kwamba jarida hilo limeshusha thamani yake kwa kipimo cha utajiri duniani Jenner ilimuuma moyo sana na kwa sasa hivi utajiri wake uko chini ya dola milioni 900″.

Aidha kwa sasa jarida la Forbes limeripoti kuwa mkataba ambao aliuweka unatarajia kuisha mwishoni mwa mwaka 2021 na utamuachia umiliki mkubwa Kim wa asilimia 72, lakini kama mama yake Kris Jenner anamiliki asilimia 8 amemzuia kuingia kufikia kiwango cha kuwa bilionea.

Aidha kutokana na mkataba mpya wa Kim’ ambao una mkakati wa muda mrefu wa kuanzisha bidhaa mpya za vipodozi vya kueneza maeneo mengi duniani imeripotiwa kuwa Kim na timu yake wamekuwa wakifanyia kazi mkataba huo wa Coty kwa miezi kadhaa.

Na taarifa hii inaweza kumvutia mume wake Kim, Kanye West ambaye alikuwa anajigamba kuhusu utajiri wa mke wakewe hivi karibuni kupitia kwenye mitandao taarifa zilizorushwa duniani kote.

 “Ninajivunia sana mke wangu mrembo Kim Kardashian kwa kuwa bilionea,” Kanye aliandika. “Umepita magumu lakini sasa Mungu amekufanya ung’ae wewe pamoja na familia yetu. Baraka hizi ziendelee kuepo katika maisha yetu.”

Mwanamuziki huyo wa miondoko ya kufokafoka aliongeza kusema; “Haya ndio maisha yetu, tunakupenda sana,” alimaliza.

Baadae Kanye alikosolewa kupitia mitandao ya kijamii kutokana na hatua yake ya kujigamba na kujinasibu kwa mali za mkewe.