NA ABOUD MAHMOUD

ZANZIBAR na Tanzania kwa ujumla kila inapotimia miaka mitano hufanya uchaguzi mkuu ambao wananchi wake huchagua viongozi kwa lengo la kuwaletea maendeleo maeneo yao wanayoishi.

Uchaguzi huo mkuu hutoa nafasi kwa wananchi waliokamilisha masharti ya upigaji kura kuwachagua viongozi mbali mbali akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Rais wa Zanzibar, Wabunge, Wawakilishi pamoja na Madiwani.

Uchaguzi mkuu unaoshirikisha vyama vingi vya kisiasa ulianza mnamo mwa 1995 wananchi na wanachama husika hulazimika kutumia haki yao ya kikatiba ya kuwachagua viongozi wanaowataka kupitia vyama hivyo.

Mwezi wa Oktoba taifa litaingia tena katika uchaguzi mkuu ambapo kwa upande wa Zanzibar inatarajia kupata Rais wa awamu ya nane ambae ataiongoza nchi hii kwa kipindi cha kwanza cha miaka mitano na kwa upande wa Rais wa Jamhuri ya Muungano atakaechaguliwa atakua Rais wa awamu ya tano.

Kwa nafasi za Ubunge, Uwakilishi na hata Udiwani wapo baadhi ya viongozi wa majimbo na wadi wanaotarajiwa kuendelea kuingia katika kinyang’anyiro hicho cha kuwania nafasi zao hizo na wapo wapya ambao nao wamejitosa katika nafasi hizo.

Naamini kila mmoja wetu anafahamu kuwa nafasi hizo zinazowaniwa na viongozi wetu watarajiwa zina madhumuni ya kwenda kuwakilisha wananchi katika vyombo vya kutunga sheria ili kuondokana na matatizo yanayowakabili katika maeneo wanayoishi au nchi kwa ujumla.

Kila inapofika wakati wa uchaguzi mambo mengi hujitokeza ikiwemo watu kutoelewana, kuhasimiana, kupigana na mambo mengi mengineyo ambayo kwa wakati mwengine hupelekea hata uvunjifu wa amani unaotokana na sababu za vyama.

Wakati umefika sasa kwa viongozi wa vyama vya siasa, dini na jamii kwa ujumla kuilinda amani tuliyonayo kwa kuinasihi jamii kutothubutu nchi kuipeleka pabaya kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.

Kwa upande wa vyombo vya habari navyo ni lazima kufuata masharti na sheria za uchaguzi na kutangaza taarifa sahihi zinazotokana na tume ya uchaguzi.

Kwa kuwa wananchi wengi huamini vyombo vya habari ndio sehemu ya taarifa sahihi hivyo havina budi kufuata maadili ya uandhishi na kucha kabisa kutoa taarifa zisizo sahihi kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu na baada ya uchaguzi.

Sambamba na hilo, alikini pia mitandao ya kijamii haina nafasi kutoa taarifa zozote zinazohusiana na uchaguzi jambo ambalo linaweza kuleta mfarakano katika nchi.

Kuvunjika kwa amani katika nchi hakutosaidia wanahabari bali litakalojitokeza ni kuleta taharuki ambayo haina faida kwa jamii na taifa kwa ujumla.

Tukumbuke ule msemo usemao kuna maisha baada ya uchaguzi, kwa maana kwamba maisha ya kawaida yanatarajiwa kurudi tena baada ya uchaguzi kama chaguzi nyengine zilizopita.

Wazanzibari na Tanzania kwa ujumla tutaendelea kujivunia amani iliyopo iwapo kila mmoja atatimiza wajibu wake ipasavyo.