NA NASRA MANZI
BENKI ya NMB imesema kuwa inathamini sana sekta ya utalii nchini na inakusudia kujikita katika harakati za kukuza shughuli za utalii.


Kauli hiyo imetolewa na Meneja wa benki hiyo kanda ya Zanzibar Abdalla Duchi, wakati wa mkutano wa wadau wa utalii Zanzibar uliofanyika katika hoteli ya Verde, mtoni Zanzibar.
Alisema benki hiyo inajipanga kutoa suluhisho la huduma za kifedha kwa kuwa na mifumo bora zaidi wa ubadilishaji fedha na biashara ya kadi.


Alisema hatua hiyo imewezesha wataliii kutohangaika wanapofanya manunuzi na malipo mbalimbali kwa kushirikiana na mahoteli na baadhi ya makampuni ya utalii kwa kugawa mashine za malipo (POS) na pia kuimarisha mfumo wa malipo ya mitandano (E-Commerce).


“Kwa Zanzibar na hata Tanzania Bara, utalii unachangia kwa kiasi kikubwa sana katika pato la taifa na kwa Zanzibar zaidi ya asilimia 80 ya fedha za kigeni katika hazina ya serikali zinatokana na utalii ndi maana nmb imeona umuhimu wa kurahisisha baaadhi ya huduma,” alisema Meneja huyo.


Alifafanua kuwa benki hiyo inaelewa kuwa katika kipindi cha maradhi ya Covid – 19 biashara kama utalii na sekta ya hoteli zilipata changamoto hivyo NMB ipo karibu zaidi na wateja wao ili kuhimili changamoto zilizojitokeza.


Alitoa rai kwa serikali na wadau wa sekta ya utalii Zanzibar kuitumia benki hiyo kwani ipo kwa ajili yao na ina mifumo thabiti ya kutoa suluhisho la huduma za huduma za kibenki inayotambuliwa na taasisi za kimataifa kuwa ndio benki bora zaidi hapa nchini kwa miaka minane mfulululizo.


Akitoa taarifa za kifedha ya benki hiyo, alisema NMB inaongoza kwa faida kwa kupata shilingi Bilioni 93.3, baada ya kodi ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 65 kipindi cha nusu mwaka 2020.


Alisema kwa mwaka huu wamefanikiwa kuleta bidhaa na fursa mpya, kwa kuzindua huduma ya bima kupitia matawi zaidi ya 220, kupitia matumizi ya mfumo wa malipo ‘QR code’ pamoja na huduma za kibenki za mitandao.