WASHINGTON,MAREKANI

KAMPUNI ya kutengeneza dawa ya Marekani ya Novavax Inc imesema kuwa inaanza utafiti wake wa kuifanyia majaribio chanjo ya ugonjwa wa Covid-19 nchini Afrika Kusini.

Kampuni hiyo ilisema kuwa inaanza majaribio hayo nchini humo kutokana na kuwepo kwa kasi kubwa ya maambukizi ya virusi vya corona.

Awamu ya 2b ya majaribio hayo ya chanjo ya Covid-19 itafanywa kwa watu wazima wenye afya wasiopungua 2,666 na itachunguza pia usalama na kinga iliyonayo chanjo hiyo kwa watu 240 wasio na maradhi, na kwa watu wazima walioathiriwa wa HIV.

Afrika Kusini ni nchi ya tano duniani kwa kuwa na idadi kubwa ya watu wenye maambukizi ya corona.

Hadi sasa jumla ya watu 583,653 waliambukizwa corona nchini humo na 11,677 walifariki kwa maradhi ya Covid-19.

Taasisi ya Bill and Melinda Gates pia ilitoa kiasi cha dola milioni 15 kwa kampuni ya Novavax Inc ya Marekani ili kusaidia majaribio hayo ya chanjo nchini Afrika Kusini.

Novavax aidha ilisema kuwa, ina mpango wa kuanzisha awamu ya pili ya majaribio hayo ya chanjo ya Covid-19 huko Marekani na Australia katika siku chache zijazo, na majariboio hayo yatawajumuisha watu waliojitolea wasiopungua 1500.