NA KHAMISUU ABDALLAH

NDUGU wawili wa familia, wamefikishwa mahakamani kwa kosa la kuvunja ukuta wa nyumba inayomilikiwa na ndugu wa aliyekuwa Makamo wa Rais wa Tanzania, Mohammed Gharib Bilal.

Ndugu hao kwa makusudi, wamedaiwa kuvunja ukuta huo ambao ni mali ya Said Gharib Bilal ilioko katika maeneo ya Chukwani wilaya ya Magharibi ‘B’ Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, majira ya saa 3:00 za asubuhi.

Wote kwa pamoja, walifikishwa mbele ya Hakimu Mdhamini wa mahakama ya wilaya Mwanakwerekwe Mohammed Subeit na kusomewa shitaka la kuharibu mali kwa makusudi.

Shitaka hilo walisomewa na Mwendesha Mashitaka, Wakili wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Mohammed Haji Kombo, ambae alidai kuwa tukio hilo walilitenda Januari 3 mwaka jana.

Alidai kuwa siku hiyo washitakiwa hao wote kwa pamoja bila ya halali na makusudi, walivunja ukuta wa nyumba unaomilikiwa na mlalamikaji Said Gharib Bilal, kitendo ambacho ni kosa kisheria.

Kosa la kuharibu mali kwa makusudi ni kinyume na kifungu cha 326 (1) cha sheria namba 6 ya mwaka 2018 sheria za Zanzibar.

Washitakiwa hao waliposomewa shitaka hilo walilikataa na kuiomba mahakama iwapatie dhamana, huku upande wa mashitaka ukidai kuwa upelelezi wake tayari umeshakamilika na kuomba kupangiwa tarehe nyengine kwa ajili ya kuwasilisha mashahidi.

Mwendesha Mashitaka, Wakili Mohammed Haji akizungumzia suala la kupatiwa dhamana kwa washitakiwa hao alisema hana pingamizi, ikiwa watakuwa na wadhamini madhubuti watakaowasimamia na kuhakikisha wanafika mahakamani kila kesi yao itakapofikishwa.

Hakimu Subeit alisema dhamana ya washitakiwa hao ipo wazi ikiwa kila mmoja atajidhamini mwenyewe kwa shilingi 1,000,000 za maandishi na wadhamini wawili, ambao kila mmoja watamdhamini kwa kima hicho hicho cha fedha za maandishi pamoja na kuwasilisha vitambulisho vyao vya Mzanzibari Mkaazi na Barua za Sheha wa Shehia wanazoishi.

Mahakama pia iliiahirisha kesi hiyo hadi Agosti 12 mwaka huu na kuamuru upande wa mashitaka kuwasilisha mashahidi siku hiyo.