BEIRUT,LEBANON

WAZIRI mkuu wa Lebanon Hassan Diab amependekeza kuandaliwa kwa uchaguzi wa mapema huku waandamanaji waliokuwa na hasira kutokana na mripuko uliotokea kwenye bandari ya mji mkuu Beirut wakivamia Wizara za serikali.

Milio ya risasi ilisikika na Ofisa mmoja wa polisi aliuawa wakati wa ghasia hizo zilizosababisha watu 238 kujeruhiwa.

Katika hotuba iliyopeperushwa kupitia televisheni,Diab alisema kuwa atawasilisha muswada wa kuandaa uchaguzi wa mapema Bungeni na kutoa wito kwa vyama vya kisiasa kukubaliana kuhusu hatua itakayofuata.

Akizungumzia kuhusu mripuko huo uliotokea mapema wiki hii, Diab alisema kuwa janga hilo ni kubwa mno na kwamba taifa hilo liko katika hali ya dharura.

Maandamano yalifikia katika hatua ya ghasia kati ya waandamanaji na polisi huku wakaazi waliokuwa na ghadhabu wakiwaomboleza waathiriwa na kutoa wito wa kuondolewa wanasiasa mafisadi.