NA TATU MAKAME
MTAZAMO finyu juu ya utoaji wa zakka kwa wananchi wenye uwezo kunapelekea wananchi wengi kutotekeleza faradhi hiyo ipasavyo, licha ya kuwapo watu wenye uwezo wa kufanya hivyo.
Ofisa Zakka na Sadaka kutoka Ofisi ya Mufti Zanzibar, Hassan Ali Kombo, alisema hayo wakati alipozungumza na mwandishi wa habari.
Alisema wapo watu wenye uwezo lakini wanashindwa kutoa zakka na kuziwasilisha ofisi husika kwa ajili ya kugaiwa kwa watu wanaostahiki katika jamii, hali inayowakosesha haki maskini ambao wanasubiri zakka kutoka Ofisi zinazohusika na ukusanyaji na kuzigawa kwa wananchi.
Alisema Ofisi zinazohusika na ugawaji wa zakka zimekuwa zikipokea maombi kwa watu wanaohitaji kusaidiwa kifedha hivyo kuwepo watu wanaoshindwa kuwasilisha michango yao kwenye ofisi hizo kunawakosesha haki watu wenye mahitaji maalum ikiwemo mafukara.
Alifahamisha kuwa mbali na elimu inayotolewa na watendaji wa Ofisi hiyo kupitia vyombo vya habari kuwataka watu wenye uwezo kujitokeza kutoa zakka, lakini mwamko umekuwa mdogo.
“Tunatoa elimu kwa wananchi juu ya utoaji wa zakka na sadaka lakini tutaongeza nguvu kwenye eneo hili ili kila mwenye uwezo aweze kutoa zakka”,alisema Ofisa huyo.