NA LAYLAT KHALFAN
MAMLAKA ya Maji Zanzibar (ZAWA), imesema utekelezaji wa miradi ya huduma ya maji safi na salama Unguja na Pemba imefikia asilimia 80.
Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Mussa Ramadhan Haji, aliyasema hayo ofisini kwake Mlandege mjini Unguja, wakati alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi.
Alisema kiwango hicho kimetokana na kuongezeka kwa miradi ya maji yenye lengo la kuimarisha upatikanaji wa huduma hiyo mjini na vijijini sambamba na kuondoa usumbufu waliokuwa wakipata wananchi muda mrefu.
Alisema hivi sasa baadhi ya maeneo ndio yanayokabiliwa na changamoto hiyo huku ZAWA ikiendelea kutatua changamoto hizo.
Alisema licha ya kuwa kuna baadhi ya maeneo ambayo hayajafikiwa ipasavyo na huduma hii, lakini jitihada zinaendelea kwa kuanzisha miradi mipya ili kuona wananchi wote wa Zanzibar wanaondokana na kadhia hiyo.
“Ingawa yapo maeneo mengine hayajaguswa moja kwa moja, lakini takriban maeneo yote hivi sasa yana miradi ambayo aidha ipo katikati, mengine karibu na mwishoni kumalizia na mengine imekamilika kwa lengo la kuwapelekea huduma hii kwa ukaribu wakaazi wa maeneo husika”, alisema.
Aidha, alifahamisha kuwa kwa upande wa wilaya za Magharibi ‘A’ na ‘B’ ni maeneo ambayo miradi ya maji ipo kwa muda mrefu lakini kutokana na ongezeko la watu na kasi ya ujenzi inasababisha kiwango cha maji kuonekana pungufu.
Alisema baada ya kuliona hilo katika wilaya hizo, serikali iliamua kwenda na miradi mipya ya maji ambayo wametiliana saini hivi karibuni na wanatarajia kuanza kufanyakazi muda wowote kuanzia sasa.
“Tuna imani kuwa kupitia mradi huu mpya hili pengo lililojitokeza la upungufu wa maji nchini basi linaondoka,” alisema.
Ofisa Uhusiano wa Mamlaka hiyo, Amina Abdallah Daud, alisema wanakusudia kujenga matangi maeneo ambayo hayana, kubadilisha mabomba na miundombinu iliyochakaa na kuweka mabomba mapya ili kuongeza upatikanaji wa huduma hiyo mjini na vijijini.
Amina aliwaomba wananchi wa maeneo mbalimbali ambayo yana upungufu wa maji kuwa na subra katika kipindi kifupi kwani wapo kutatua kero hiyo ili kuhakikisha huduma ya maji safi na salama inafikiwa ipasavyo.