LONDON, England
KIUNGO wa Arsenal, Mesut Ozil amerejea tena kwenye vyombo mbalimbali vya habari, akizungumzia sakata lake la kugoma kupunguziwa mshahara kama sehemu ya kuendana na madhara ya mripuko wa ‘corona’ duniani.
Klabu mbalimbali ulimwenguni zilipendekeza wachezaji wake kupunguziwa mishahara ili waweze kukidhi mahitaji ya kifedha za uendeshaji wa timu hizo. Arsenal ni moja ya timu iliyopendekeza na kutekeleza utaratibu huo.
Mengi yalizungumzwa kuhusiana na Ozil kugoma kupunguziwa mshahara wake, lakini, pia taarifa kutoka kwa mwenyewe hazikusikika.
Akizungumza na Athletics, Ozil, alisema: “Kama wachezaji, tulitaka kuchangia. Lakini tulihitaji taarifa zaidi na tulikuwa na maswali mengi ambayo hayakujibiwa”.
“Ningekuwa tayari kuchukua hisa kubwa na pengine kukatwa mshahara kama ilipaswa kuwa hivyo mpaka pale mpira na hali ya kiuchumi ikiwa sawa. Lakini tulilazimishwa kufikia uamuzi huo bila ya kuwa na majadiliano thabiti”.
“Kwa yeyote ambaye angekuwa kwenye hali hii, anahaki ya kujua kila kitu, kujua kinachofanyika na ni wapi fedha zinakwenda.”
“Hatukupewa taarifa za kutosha, tulielekezwa kufanya maamuzi tu. Ilikuwa ni mapema mno kwa kitu ambacho kilikuwa ni muhimu na chenye msukumo mkubwa”.
“Hii haikuwa sawa, hasa kwa wachezaji wadogo, na nilikataa. Nilipata mtoto na nina hudumia familia hapa Uturuki na Ujerumani na kwenye shughuli zangu za misaada. Nina mradi mpya wa kuwasaidia watu wa London, yale ni maamuzi yangu kutoka moyoni, sio kwa ajili ya kufurahisha watu”.
Ozil alitajwa kama mchezaji pekee wa Arsenal aliyekataa kupunguziwa mshahara katika kikosi cha Arsenal.